UTAFITI: Uwekezaji baharini chanzo samaki kuadimika...soma habari kamili na Matukio360..#share
Na Mwandishi wetu
WAKATI Tanzania ikikabiliwa
na uhaba wa kitowewo cha samaki kwa siku za karibuni utafiti umeonesha uwekezaji katika bahari kama kutafuta mafuta
na gesi ni shughuli zinazochochea samaki kupotea au kwenda kwenye kina kirefu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi za Maji na Uvuvi,Dk Benaisha Benno
Pia asilimia 90 ya wavuvi
nchini kutumia zana duni hali inayopelea kuvua samaki tani 52,000 kwa mwaka
ambao ni kidogo tofauti na rasilimali zilizopo kwenye bahari ya Hindi.
Hayo yamesemwa na mhadhiri
wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi za Maji na Uvuvi,Dk Benaisha
Benno alipokuwa akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya uharibifu wa
mazingira kwenye bahari uliondaliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira la
Umoja wa Mataifa (WWF).
"Bahari kwa sasa
inakutana na changamoto nyingi kama uharibifu wa matumbao, kukata mikoko na
kutafuta mafuta na gesi hali ambayo inakimbiza samaki katika kina kifupi na
kwenda kina kirefu," amesema Dk Benno.
Benno amesema wavuvi hao
hawana vifaa vya kisasa vitakavyowasaidia kuvua samaki katika bahari kuu
matokeo yake wanashindwa kuvua samaki wakubwa na wengi ili waweze kujipatia
kipato cha kuendeshea maisha yao.
Amesema sekta ya uvuvi
ikitumika kikamilifu itakuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi na wananchi.
"Tafiti ambayo
ilifanyika 2014 inaonesha asilimia 90 ya wavuvi wanatumia dhana duni hali
ambayo inasababisha washindwe kwenda kwenye kina kifupi hivyo wanapata samaki
wachache," amesema.
Dk. Benno alisema kutokana
na dhana duni wavuvi wameshindwa kuvua katika kina kirefu ambacho ni mita 200
hivyo wanakosa samaki wakubwa kama jodari.
Amesema ni wakati muafaka
kwa serikali kuwekeza katika sekta hiyo ili kuhakikisha rasilimali zilizopo
baharini zinatumika kwa usahihi.
Kwa upande wake Mtafiti
Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tazania(Tafiri),Baraka Kuguru amesema
sekta ya uvuvi ikipewa kipaumbele itachangia ukuaji wa uchumi na hivyo
kutekeleza malengo ya viwanda na uchumi wa kati.
Kuguru amesema tafiti
ziaonyesha kuwa sekta ya uvuvi imekuwa na mchango mkubwa kwa nchi ambazo
zimewekeza hasa katika ukanda wa bahari ambapo rasilimali zilizopo kwenye
bahari zina thamani ya dola za Marekani 333 bilioni huku uwekezaji ukiwa
asilimia 20 mpaka sasa.
Dk Kuguru amesema pamoja na
wavuvi kuwa na vifaa duni vya kuvulia ipo changamoto nyingine ya kuharibu
mazalia ya samaki kama matumbao na mikoko hali ambayo inaweza kuchochea uvuaji
samaki kupungua.
Akizungumza katika mafunzo
hayo Meneja Kampeni ya kulinda Hifadhi ya Selous kutoka WWF, Atilio Tegalile
alitoa rai kwa wanahabari kujikita katika habari za mazingira na bahari ili
kuweza kusaidia nchi na wananchi hasa wanaojihusisha na uvuvi.
Meneja huyo amesema iwapo
kutakuwa na kundi la wanahabari waliojikita kuandika habari za utunzaji
mazingira na rasilimali za habari kutakuwa na mabadiliko chanya hivyo dhana ya
uchumi wa viwanda itatekelezeka kirahisi.
"Natumia nafasi hii
kuwaomba mjikite katika uandishi wa aina moja (specialization) kwani ndio
uandishi wa sasa na mtapata tuzo, " amesema.
Mmoja wa wavuvi wa soko kuu
la samaki la Zanzibar, Hamisi Arafat Hamisi ameiomba serikali iwatengenezee
mazingira bora yatakayowawezesha kupata mikopo ili waweze kununua vifaa vya kisasa vitavyoweza kufika
bahari kuu ambapo wataweza kuvua samaki aina ya jodari na papa.
Kwa upande wake Mvuvi Omary
Hamis amesema changamoto iliyopo ni ukosefu
wa boti yenye uwezo wa kuvua katika kina kirefu hali inayosababisha kuvua
samaki wadogo na wachache.
"Boti tunazotumia
zinaweza kuvua mita isiyozidi 30 hivyo kupelekea kupata samaki wachache na
wadogo,tunaiomba Serikali isifikilie kuchukua kodi ijikite kwenye uwekezaji wa
sekta ya uvuvi kwani ina faida kwa nchi na wananchi,alisema Hamisi.
No comments:
Post a Comment