Wabunge waibua hoja dhidi ya wateule wa JPM..Soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Mwandishi Wetu

WABUNGE wameibua hoja ya nani ni kiongozi mkubwa kwa cheo kati ya wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa .
Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hoja hiyo imeibuka leo mjini Dodoma katika semina ya wabunge wa kamati mbili za Bunge kuhusu masuala ya kidiplomasia na itifaki ambayo imeandaliwa  na Bunge kupitia Mradi wa Kujengea Uwezo Wabunge na Wawakilishi unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).

Aidha washiriki katika semina ni wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na wawakilishi kutoka vyama vya kibunge.

Akichangia katika semina hiyo Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hillal ametoa mfano wa ziara za kikazi akisema mbunge huwekwa wa mwisho, akitanguliwa na mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya.

“Unakuta mkoa katika ziara gari la mbele yupo RC ameweka bendera, linalofuatia ni la DC naye ameweka bendera na la mbunge linakuwa nyuma. Tunaomba utufafanulie katika hilo,” amesema.

Kwa upende wake Mbunge wa Morogoro Kusini-Mashariki (CCM), Omary Mgumba amesema mkuu wa wilaya anamwakilisha Rais na katika wilaya nyingine huwa zina majimbo mawili ya uchaguzi, hivyo kumfanya mbunge kuwa na eneo dogo la kiutawala ikilinganishwa na mkuu wa wilaya.


“Siku zote ukweli ni mchungu na hasa ukiwa hutaki kuusikia. Utakuta wilaya moja ina majimbo mawili, mbunge wa jimbo moja utawala wake ni kwenye jimbo lake tu lakini mkuu wa wilaya ni mtawala katika majimbo yote mawili yaliyo katika wilaya yake,” amesema.

Akizungumzia hilo, Mbunge wa Mtambile (CUF), Mosoud Abdallah, amehoji itifaki inazungumzaje kuhusu mbunge wa jimbo na wa viti maalumu wanapokuwa jimboni.

“Tunapokuwa jimboni ni mbunge gani anakuwa mkubwa kwa cheo kati ya mbunge wa viti maalumu na wa jimbo,” amehoji.

Akijibu hoja hizo, ofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Kitengo cha Uhusiano wa Kimataifa, Ally Masabo amesema kiitifaki mkuu wa mkoa ndiye mwenye mamlaka katika mkoa, hivyo ndiye anayetakiwa kuwa mbele katika msafara mkoani.

"Suala hili wabunge wana wajibu wa kuangalia, na utatuzi upo kwenu wabunge," amesema Masabo ambaye ametoa mada katika semina hiyo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search