Wananchi, askari watunishiana misuli...Soma habari kamili na Matukio360
Na Salha Mohamed
NI kama filamu inaanza. Askari wakiwa na silaha za moto
wakiwa barabarani huku wananchi wakiwa wanapiga kelele na kulalama wakidai
wanataka haki zao.
Askari wa Jesho la Polisi na Wakazi wa Ukonga Mombasa jijini Dar es Salaam wakisubiri kumsikiliza Mkuu wa Wilaya Ilala Sophia Mjema.
Ndivyo imekuwa leo kwa wakazi wa Ukonga Mombasa eneo la
Mazizini jijini Dar es Salaam, baada ya wananchi kufunga barabara kwa kile
kinachodaiwa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), Ukonga kupiga na
kujeruhi raia.
Oktoba 22 mwaka huu, eneo la Ukonga Mombasa, majira ya saa mbili
usiku askari hao walianza kupiga kila raia aliyepo eneo hilo bila kujali
umri, jinsia wala hali ya mwananchi.
Kupigwa kwa wananchi hao imedaiwa ni kulipa kisasi kwa kuuawa
kwa askari mwenzao, PC Charles Yanga.
Kifo cha askari huyo kilitokea Oktoba 21, mwaka huu ambapo
mwili wake ulikutwa ukiwa kiwa na majeraha kwenye paji la uso na sikio
moja likiwa limekatwa kabisa ukiwekwa pembeni mwa uzio wa kambi yao ukiwa
ameanguka chini huku pikipiki yake aliyokuwa akiendesha ikiwasha taa za
tahadhari (hazards light).
Kutokana na tukio hilo, askari hao waliingia eneo hilo
nakuanza kumpiga kila raia wanayemuona mbele yao kwa rungu, mkanda na hata
mateke na kuwasababishia majeraha makubwa na hata kuwavunja viungo (mguu).
Jambo hilo liliwafanya wananchi hao kukimbia hovyo na kufunga
biashara zao mapema kutokana na hofu waliyokuwa nayo kwa kile kipigo
wanachokiona au kukipata kwa askari hao.
Kipigo hicho hakikuwafurahisha wananchi jambo
lililowasababisha kufunga barabara ya Mazizini hadi Moshi Bar kwa saa kadhaa
huku wakidai amani kwani wameharibiwa mali zao huku wengine wakidai
wameharibiwa kisaikolojia.
Baada ya kufungwa kwa barabara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wilayani hapo, Sophia Mjema
alifika eneo hilo na kuwasihi askari hao(FFU) kuondoka eneo hilo.
Baada ya askari hao kuondoka ndipo wananchi walipoanza kupaza
sauti zao kwa kudai wameumizwa na pindi wanapokwenda polisi kuomba PF3 ili
wakapate matibabu hukataliwa.
Mjema aingilia kati Kutokana na vurugu hizo na shughuli za
kibiashara kusimama eneo hilo, Mjema amewataka wananchi hao kuwataka
askari waliohusika katika vurugu hizo ambapo watachukuliwa hatua kama
kuhamishwa kikosi.
Wananchi hao walisema wanawafahamu askari waliokuwa
wakiwapiga huku wakipaza sauti zao kwa kulitaja jina la askari mmoja
aliyefahamika kwa JJ ambapo alichukuliwa kijana aliyejulikana kwa kwa jina
la Jamal Yahaya kuwataja askari hao.
Wakazi wa Ukonga Mombasa wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ilala (pichani hayupo)
Mjema amesema hakubaliani na kitendo cha askari hao kuwapiga
raia kwami haijajulikana sababu ya kifo cha askari huyo.
"Jambo hili halikubaliki kama kuna tatizo lolote ambalo
askari wanaliona kuna ngazi na taratibu za kisheria, wao kujichukulia sheria
mkononi haikubaliki. Lazima hao askari waliofanya hivyo wachukuliwe hatua
za kinidhamu na kisheria,"amesema.
Amesema wananchi walioharibiwa mali zao, walioumia
wajiorodheshe ili waweze kuoata matibabu na mali zao."Wananchi watulie hili
jambo si kubwa sana hadi wakoseamani lipo ndani ya uwezo wa serikali ya Wilaya
wananchi watulie,"amesema.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Kata ya
Mazizini, Richard Muhuza amesema aliwaona askari na kuwasihi kuacha
kuwapiga wananchi lakini alishindwa kutokana na askari hao kuwa wengi.
"Askari walikuwa wamevaa soksi nyeusi, sare za jeshi,
bukta, pensi wapo zaidi ya 50 walikuwa wanaingia hadi ukumbini kwenye
sherehe wakisema tunawapiga wote hakuna cha sherehe kwanini askari mwenzao
ameuawa.
"Walikuwa wanampiga kila mtu anayeshuka kwenye daladala,
upo nyumbani umeacha mlango wazi wanakupiga na kuchukua fedha, sisi
tulishindwa kwasababu walikuwa wengi wanamarungu bakora hawajui huyo mtoto
wao wanapiga tu,"amesema.
Polisi walaani
Jeshi la Polisi Kanda hiyo, limelaani vikali vitendo hivyo
ambavyo havina maadili ya kazi za Polisi huku likifungua jalada na uchunguzi
kunaendelea ili kuwabaini watuhumiwa wa tukio hilo.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo,SACP Lazaro Mambosasa amesema
“Tunaomba wananchi watoe ushirikiano kutoa taarifa za wahusika ili kuwachukulia
hatua watu au askari waliohusika na matukio hayo ya kuwapiga wananchi kitendo
ambacho ni kinyume na sheria za nchi,"amesema.
Amesema katika ufuatiliaji Polisi wamebaini askari huyo
kauwawa na watu wasiojulikana kisha kutelekezwa katika maeneo hayo
ya kambi ya Polisi.
"Polisi kupitia kikosi kazi chake kinaendelea na msako
mkali wa ufuatiliaji wa tukio hili la kinyama ili kuwabaini watuhumiwa waliohusika
kutekeleza mauaji hayo na kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili,"amesema.
Wakati huo huo, Jeshi hilo limepokea malalamiko ya watu
wanaosemekana ni askari kufanya msako na kuwapiga wananchi wanaoishi
maeneo ya jirani na kambi ya Polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) ambao
hawana hatia yeyote.
No comments:
Post a Comment