Waziri Mwakyembe ateta na viongozi wa dini...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Hussein Ndubikile
VIONGOZI wa Madhehebu ya Dini nchini wametakiwa kuwakemea waamini wao waache kuvaa mavazi yasiyofaa wakiwa madhahabuni badala yake wawafundishe matendo mema yanayompendeza Mungu na yanayodumisha maadili na uzalendo wa nchi.

Waziri Dk Mwakyembe akiwa na viongozi wa dini
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe katika mkutano uliomkutanisha na Viongozi wa Madhehebu ya dini kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.
Amesema maadili ya jamii yamekuwa yakimomonyoka kutokana viongozi hao kuyafumbia macho hata pale kwenye nyumba na kwamba wanatakiwa kuwakemea kwa kuwafundisha yale yote yanayomchukiza na kumpendeza Mungu.
“ Viongozi wote wa dini mnatakiwa kukemea waamini wasivae mavazi yasiyofaa kimaadili siku zote matatizo makubwa yanaanza polepole tukichelelwa kuwakumbusha waamini na vijana wetu wanapotea,” amesema.
Amebainisha kuwa viongozi wanatakiwa kuwakumbusha waamini wajibu wa kulipa kodi, kufanya kazi kwa bidii, kutunza mazingira, uaminifu, uadilifu, uwajibikaji na kutii mamlaka na kulinda rasilimali za nchi.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kutoa lugha za kichochezi lengo likiwa kuiokoa nchi isiingie kwenye janga la machafuko kama yanavyotokea katika mataifa mengine ya Afrika.
Amewapongeza wasanii wa nyimbo za Injili na Kaswida kwa kutumia lugha sanifu na kuvaa mavazi ya staha wakiwa kazini.
Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amewahimiza viongozi wenzake kutoyanyamazia  maovu huku akiongeza mwenyezi Mungu humpenda mtu anayetenda mema.
Naye Mchungaji Antonio Fernandes ambaye pia ni Mmiliki wa Kituo cha Runinga cha ATN amesema kila mwananchi ana wajibu kufanya kila ili kujiletea maendeleo na kuikomboa nchi kiuchumi.
Ameiasa jamii kuacha kuitumia vibaya mitandao ya kijamii vibaya badala yake waitumie kutafuta fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye mitandao hiyo.
Mlezi wa Jumuiya na taasisi za madhehebu ya dini, Mary Rhoida amewakumbusha viongozi kuwa na utaratibu wa kutatua migogoro  katika ngazi za chini ili kuepuka migongano inayoweza kujitokeza.
Mwakilishi kutoka Rita, Lina Msangi amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuwasisitiza na kuwakumbusha waamini wao kuwa na utamaduni wa kushughulikia vyeti vya kuzaliwa na kufuatilia masuala ya mirathi.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search