Waziri Ummy apokea vifaa vya saratani...soma habari na Matukio360..#share
Na Abraham Ntambara
TANZANIA inakabiliwa na changamoto ya kuwa na ongezeko la idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na saratani.
WAZIRI na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Dk. Faustine Ndugulile (wapo katikati) wakikabidhi vifaa tiba walivyopokea kwa Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili ya kusambazwa katika vituo vya afya.
...
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam wakati akipokea vifaa vya uchunguzi na matibabu ya
awali ya saratani ya mlango wa kizazi, waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema takwimu zinaonesha kila mwaka takribani
wagonjwa wapya 50,000 wanagundulika kuwa na saratani.
Vifaa hivyo ni mashine 100 za tiba mgando (cryotherapy) na mashine tisa za upasuaji mdogo (LEEP) ambazo zitatumika kwa ajili ya matibabu ya awali ya saratani kwa wanawake watakaofanyiwa uchunguzi na kukutwa na mabadiliko ya awali ya saratani hiyo.
“Idadi hii inakadiriwa itaongezeka kwa asilimia 50 ifikapo 2020,” amesema Ummy.
Tarifa kutoka Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road kwa kipindi cha mwaka 2006 hadi 2015 zinaonyesha kwamba
aina za Saratani zinazoongoza nchini ni Saratani ya mlango wa kizazi asilimia 34, Saratani ya
Ngozi (kaporsis Sarcoma) asilimia 13 na Saratani ya matiti asilimia 12.
Nyingine ni Saratani ya mfumo wa
njia ya chakula asilimia 10, Saratani ya Kichwa na shingo asilimia 7, Saratani ya Matezi asilimia 6, Saratani ya Damu asilimia 4, Saratani ya Kibofu cha mkojo asilimia 3, Saratani ya
ngozi asilimia 3, Saratani ya Macho asilimia 2, na saratani ya tezi dume asilimia 2.
Amesema kutokana na takwimu hizo asilimia
80 ya wanawake wanaougua saratani hii wanafika katika vituo vya kutolea huduma
za afya kwa ajili ya tiba wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa, ambapo
hufanya matibabu kutokuwa na matokeo mazuri.
Ameongeza kwamba Serikali imekuwa
ikitumia fedha nyingi kutibu wagonjwa hao ambapo ameeleza kuwa Saratani
ya Mlango wa kizazi inatibika endapo itagundulika mapema sambamba na kusaidia
kupunguza gharama za matibabu ambazo Serikali, familia na mgonjwa wamekuwa
wakikabiliana nazo.
Waziri Ummy amesema Kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali, Wizara imeshaanzisha vituo 459 (vituo 343 vya
serikali na 116 vya mashirika na watu binafsi) vinavyotoa huduma ya uchunguzi
na matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.
Akizungumzia kuhusu vifaa
alizopokea, amesema huo ni mkakati wa serikali Katika kuhakikisha inaongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi
na matibabu ya awali ya Saratani ya Mlango wa Kizazi.
Amewatoa hofu watanzania kuhusu gharama za matibabu kwa kusema kuwa huduma hizo zinapatikana katika Hospitali zote za Rufaa za Kanda na Mikoa, Hospitali zote za Wilaya, na baadhi ya Vituo vya Afya na Zahanati bure na kuwataka waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatoa huduma hizo bila vikwazo.
No comments:
Post a Comment