Zitto; Serikali 'inapika' Takwimu pato la taifa(GDP)...soma habari kamili na Matukio360...#share

Na Saha Mohamed
KAMATI Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, imesema takwimu za ukuaji wa pato la taifa(GDP)zimepikwa  na si sahihi kama ambavyo taasisi za serikali zikidai.

Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe
 Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe wakati akiwasilisha ushahidi kuhusu kusinyaa kwa uchumi wa nchi.

Amesema Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG), anapaswa kufanya ukaguzi wa mapato ya serikali kwa Julai na Agosti mwaka  huu na kuiweka wazi kwa umma.

Amesema mbali na CAG kufanya ukaguzi pia Mamlaka ya Mapato (TRA) ieleze mapato yake kwa kila idara pamoja na kuonesha marejesho na madeni yatakayokusanywa kama mapato.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kigoma mjini amesema Jumuia za Afrika Mashariki, Benki ya Maendeleo ya Afrika na Benki ya Dunia kufanya uchunguzi maalumu wa takwimu za uchumi nchini.

“Hatua kali zichukuliwe dhidi ya serikali ya awamu ya tano ikigundulika kuwa takwimu juu ya ukuaji wa pato la taifa zimepikwa,”amesema zitto.

Ameongeza kuwa Serikali inapaswa kubadilisha sera zake za matumizi kwa kuhakikisha miradi mikubwa inayotekelezwa nchini inaingiza fedha nchini na si kupeleka fedha nje ya nchi kama ambavyo imenunua ndege 6 kwa fedha taslimu.

Amesema kwa kufanya hivyo kunaonesha madhara kwenye uchumi kwasababu badala ya kuongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi unafanya uchumi kusinyaa.

Amesema Pato la taifa ndiyo kipimo cha afya au uhai wa uchumi wa taifa  kwani ukuaji au uporomokaji wake hutumika kupima shughuli za kiuchumi za taifa husika.

Ameongeza kuwa tafiti zinaonesha ili kuondokana na umasikini wa nchi, uchumi unatakiwa ukue kwa kiwango cha tarakimu mbili kwa miaka mitano mfululizo kiwango hicho hakijawahi kufika.

Amesema wastani wa  ukuaji umekuwa kwa asilimia 7 huku katika mzunguko wa fedha kwa miaka mitano iliyopita umekuwa kati ya asilimia 0.5 na 1.5.

Zitto amesema kiwango hicho hakitofautiani na kiwango ambacho Benki Kuu ya Ulaya(ECB)imeweka kama mzunguko wa ujazo wa fedha kwa nchi zote za Umoja wa Ulaya(EU).

Amefafanua kuwa takwimu za mwaka 2014 hadi 2016 za ukuaji wa GDP robo ya pili Aprili hadi Juni ya kila mwaka zimekuwa zikishabihiana.

“Hali hiyo imekuwa tofauti mno kwa robo ya pili ya mwaka 2017, utofauti ambao mdiyo msingi ulioibua shaka na kusababisha utafiti huu,”amesema.

Amesema robo ya pili ya mwaka 2017 Benki ya Kuu(BOT) imetoa takwimu za ukuaji wa GDP kwa robo inayoishia Juni 2017 kukua kwa kasi ya asilimia 5.7 na mfumuko wa bei asilimia 6 ambapo kasi hiyo unatofautiana na mlinganisho wa kanuni za kiuchumi.

“Mtakubaliana name kuwa takwimu  za pato la taifa kwa robo inayoishia Juni 2017 si takwimu sahihi, hazikubaliani na nadharia ya uchumi na zimetofautiana sana na miaka minne ya nyuma,”amesema.

Zitto ameongeza “Takwimu hizi zimepikwa ili kuonesha picha kua hali ya uchumi ni nzuri ilhali uhalisia ni kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi imeporomoka mno,”amesema.

Amesema kwa miezi kadhaa wamekuwa wakipiga kelele kuwa kitendo cha serikali kuminya sekta ya fedha na hasa kwa sekta binafsi.

Ameongeza kuwa takwimu za makusanyo ya kodi za serikali kutoka TRA, zinaacha mashaka makubwa kwa kila mtaalamu wa uchumi na kuamini kuwa ni za kutengezezwa.

“Julai, serikali ilikusanya sh bilioni 390 kutoka kodi za forodha, lakini Julai serikali haikuwa na takwimu za biashara ya kimataifa kwa sababu mfumo wa forodha ya pamoja katika EAC.

“Je serikali imewezaje kupata takwimu za kodi bila takwimu za biashara?kodi inatoka kwenye bidhaa zilizoingizwa nchini hivyo ili kupata kodi lazima kupata bidhaa kwanza,ni dhahiri serikali inaficha takwimu hizi makusudi ili kuzuia kuonesha kuwa mapato yameshuka,”amesema.

 

                    





About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search