Hakimu atoa onyo kesi vigogo Rahaco...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Abdulrahim Sadiki
 MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa onyo la kuifuta kesi ya kuisababishia serikali hasara ya  dola za Marekani  527,540, inayowakabili vigogo wa kampuni hodhi ya mali za reli (Rahaco) kwa kiwango ambacho washtakiwa hao hawatakamatwa tena.


Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba ametoa onyo hilo baada ya ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kuomba siku 14 ili kukamilisha utaratibu wa kupeleka taarifa za kesi  hiyo, Mahakama Kuu.
Ombi hilo lilitolewa jana na mwendesha mashtaka wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuru), Mghela Ndimbo

Kufuatia  maelezo hayo, Hakimu Simba alitoa ahirisho la mwisho na kuwaeleza kuwa ataifuta kesi hiyo kwa kiwango ambacho washtakiwa hao hawatakamatwa tena. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 16,2017

 Washitakiwa hao ni mkurugenzi mtendaji, Benhardard Tito, mwanasheria wa Rahaco, Emmanuel Massawe na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane ya uhujumu uchumi likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kusababisha hasara ya dola za Marekani 527,540.

Washtakiwa hao wadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa walikula njama kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,  Tito, anadaiwa kuwa  Februari 27, 2015 katika ofisi za Rahaco zilizopo Ilala alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahaco.

Tito na Massawe wanadaiwa kuwa Machi 12, 2015 katika ofisi za Rahaco Ilala wakiwa katika nyadhifa zao, walisaini barua ya kuihalalisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi huo.

Tito na Massawe wanadaiwa kuwa  Machi 12 na Mei 20, 2015 wilayani Ilala walishindwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini na Rahaco.

Tito na Massawe wanadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi za Rahaco, kwa kutumia madaraka yao vibaya walisaini mkataba wa kutoa huduma za ushauri na kampuni ya Afrika Kusini bila ridhaa ya Bodi ya Zabuni ya Rahaco.

Washtakiwa hao, wanadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kuwasilisha mkataba walioingia na kampuni ya Afrika Kusini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tito, Mwinyijuma na Massawe, wanaodaiwa kati ya Machi mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi za Rahaco, waliipa kazi kampuni hiyo ya ushauri na kuilipa kwa kutoa huduma za ushauri, malipo ambayo yaliisababishia Rahaco kupata hasara ya dola za Marekani 527,540.

Tito anadaiwa Agosti 18, 2015 katika ofisi za Rahaco Ilala, ambapo kwa kutumia madaraka yake vibaya aliipa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China kazi ya kujenga kilomita mbili za reli maeneo ya Soga iliyogharimu dola za Marekani 2,312,229.39 bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahaco.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search