Kesi ya Halima Mdee mhh!!!..soma habari kamili na Matukio360..#share

Na Abdulrahim Sadiki
KESI ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya rais, Dk John Magufuli inayomkabili mbunge wa jimbo la Kawe(Chadema), Halima Mdee imeshindwa kuanza  kusikilizwa kufuatia  shahidi kuanza  likizo na anasafiri.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kulia akiwa na mmoja wa mawakili wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakili wa serikali, Leonard Challo amemueleza Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa  kesi hiyo ilipaswa kuanza kusikilizwa leo  lakini  shahidi waliyemtarajia kuanza kutoka ushahidi   ameanza likizo na  anasafiri.

Ameomba  ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikilizwa na siku hiyo wataleta shahidi mwingine. 

Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 7,2017  kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka. Hatua hiyo imefikiwa baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Katika usomwaji wa maelezo ya awali ya kesi hiyo (PH), Halima alikumbushwa shtaka linalomkabili,   kuwa alifanya kosa hilo Julai 3,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) iliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni.

Kwa  kumtukana rais John Magufuli  kuwa “anaongea hovyo hovyo , anatakiwa  afungwe breki,” kitendo ambacho kingeweza  kusababisha uvunjifu wa amani.

Akisomewa maelezo ya awali, Halima alikubali maelezo yake binafsi likiwamo jina lake, anaishi Makongo, yeye ni Mbunge na Siku ya tukio ya Julai 3,2017 alikuwa katika eneo la ofisi ya Chadema iliyopo mtaa wa Ufipa Kinondoni. Halima alikana kutoa lugha ya matusi dhidi ya rais Dk John Magufuli.

Akiendelea kusomewa maelezo hayo ya awali,  Halima alikubali kuwa Julai 4,2017 alikamatwa katika eneo la Kibangu wilaya ya Kinondoni na  kupelekwa katika ofisi ya ZCO kwa mahojiano.

Hata hivyo, Halima alikana maelezo ya kuwa wakati akihojiwa alikubali kuwa alitoa lugha ya matusi dhidi ya rais Magufuli. Pia Halima alikubali kuwa alifikishwa mahakamani kukabiliana na kesi inayomkabili. Alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Julai 10,2017.

Katika kesi hiyo anatetewa na mawakili, Peter Kibatala, Nashon Nkungu, Jeremiah Mtobesya, Faraja Mangula, Omary Msemo, Hekima Mwasipu.

Tayari Mdee kupitia mawakili wake amewasilisha pingamizi la awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yake ya kumtolea lugha chafu rais Magufuli.


Wanadai mapingamizi mawili, kwanza hati ya mashtaka ina mapungufu, pia Mahakama hiyo haina mamlaka akisema kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka kwa sababu, Mkuu wa Wilaya aliyetoa amri ya kukamatwa kwa Mdee ameshindwa kufuata matakwa ya kisheria.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search