Waziri Mkuu: Katiba mpya bado, amzungumzia Tundu Lissu...soma habari kamili na Matukio360..#share

Na mwandishi wetu
SERIKALI imesema kwa sasa mchakato wa kuendelea na upatikanaji wa katiba mpya si kipaumbele chake kwa kuwa unahitaji fedha nyingi.

Msimamo huo umetolewa leo Bungeni Dodoma na waziri mkuu, Kassim Majaliwa katika kipindi cha maswali na majibu ya ana kwa ana na waziri huyo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akijibu majibu Bungeni Dodoma

Akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea kuhusu Katiba mpya, waziri mkuu amesema kwa sasa kipaumbele cha serikali ni  kuboresha huduma za jamii .

‘Tatizo ni kuwa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya unahitaji fedha nyingi na  kwa sasa kipaumbele cha serikali ni kuboresha huduma za jamii, hivyo haiwezi kuratibu suala hilo,’ amesema

Amesema suala hilo pia linashindikana  kutokana na bajeti ya mwaka 2017/18 haikuelekeza wala kutoa kipaumbele  kwenye mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

Kuhusu upelelezi wa tukio la upigwaji risasi mbunge Tundu Lissu amesema suala hilo bado linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya usalama vya ndani na kwamba serikali kwa sasa haiwezi kuruhusu vyombo vingine vya nje kuchunguza suala hilo.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Hai(Chadema) Freeman Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti taifa wa chama hicho, aliyetaka serikali kuruhusu vyombo huru kutoka nje ya Tanzania kuchunguza tukio  hilo.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa hawezi kutoa uamuzi wowote  hadi hapo vyombo vya usalama vitakapomaliza uchunguzu na kutoa mapendekezo yao.

Kuhusu zao la mbaazi, waziri mkuu amesema serikali inaendelea na jitihada za kutafuta masoko na kwamba ilikuwa ikitegemea nchi ya India pekee kununua zao hilo.


‘Lakini kwa mwaka huu India imezalisha ziada ya asilimia 30 ya mbaazi hivyo imezuia kununua mbaazi kutoka nje. Lakini pamoja na changamoto hiyo serikali inaendelea kutafuta soko mahala pengine,’amesema

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

1 comment

  1. Binafsi, ninahoji majibu ya Waziri Mkuu. Hii hoja ya gharama kuhusiana na katiba mpya nina mashaka nayo. Ingekuwa serikali ina uchungu na hela za walipa kodi, mbona haisemi ni gharama kuwadhibiti wapinzani wanapotaka kutumia haki zao kwa mujibu wa katiba na sheria? Mpinzani akiikosoa serikali, hata kama yuko mbali kiasi gani, anatafutwa na magari ya polisi wenye silaha na kubebwa hadi kituoni. Wapinzani wakikusanyika kwa mujibu wa katiba na sheria ya vyama, mabomu ya kuwatawanya yako tele, hata kwenye miji midogo. Magari ya maji ya washawasha ya kuwatawanya yako tele. Mafuta ya haya magari, spea za haya magazi, posho za madereva na polisi, nazo si gharama? Hao watu wanaoitwa wachochezi wanafunguliwa kesi kila kukicha, kesi ambazo wanashinda, kwa sababu hazina vichwa wala miguu. Lakini hela za walipa kodi zinafujwa katika kesi hizo. Ufujaji huu wa hela unaofanywa na serikali unanifanya niwe na mashaka na hoja ya waziri mkuu kuhusu gharama ya kuendelea na mchakato wa katiba mpya.

    Kuhusu suala la uchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu, nimesikia kuwa familia ya Tungu Lissu, pamoja na kuwa wanataka wachunguzi wa ndani wafanye hiyo kazi, wanataka wachunguzi wa nje washirikishwe. Serikali itumie busara kwenye suala hili. Ili kuondoa mashaka na tuhuma dhidi yake, ni busara kujumlisha wachunguzi wa nje. Itaondoa wingu lot. Ila kama serikali haijali minong'ono na hisia dhidi yake, basi iendelee hivyo inavyotaka.

    ReplyDelete

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search