Uwanja mpya wa ndege kujengwa zanzibar ...Soma habari kamili na Matukio360...#share

WAZIRI wa Fedha na  Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed amesema ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege unatarajiwa kuanza tena  Disemba Mwaka huu chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  kupitia Exim Bank.
Waziri wa Fedha na  Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed.

Amesema ujenzi wa  jengo jipya ni miongoni mwa miradi  mitatu mikubwa ya maendeleo katika kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume kiliopo Kisauni ambacho kinaumuhimu mkubwa kwa uchumi wa  Zanzibar.

Ameyasema hayo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Vuga  alipokuwa  akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu changamoto zilizojitokeza ambazo zilisababisha kushindwa kukamilika  kwa ujenzi huo .

Amesema kutokamilika kwa muda mrefu jengo jipya la kuhudumia abiria kulipelekea changamoto ya kumudu kuhudumia ndege kubwa aina ya Code E kulingana na mahitaji ya sasa na uwezo wake wa idadi ya abiria wataohudumiwa kwa mwaka .

Waziri huyo amesema utengenezaji wa jengo utaligana na mahitaji mapya ya shirika la usafiri wa anga la duniani (ICAO) na mkabala wake wa maeneo ya kuegesha ndege yaliojengwa kwa ufadhili wa benki ya dunia .

Ameeleza kutokana na kadhia hiyo Serikali ililazimika  kuajiri mshauri maalumu kutoka kampuni ADPi kutoka ufaransa ili kuweza kuishauri vizuri juu ya utatuzi wa changamoto zilizobainika  .

Hata hivyo amesema marekebisho yaliyopendekezwa na kukubaliwa na Serikali yalipelekea kuongezeka kwa gharama za mradi kutoka dola 70.4 millioni hadi 128.7 million .

Alieleza gharama hiyo ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo lenyewe eneo Zaidi la maegesho ya ndege la mita za mraba 38,000 na eneo la kuegesha gari za watumiaji wa uwanja ,abiria pamoja na wapokeaji abiria .

Waziri wa fedha amesema tatizo hasa lililojitokeza ni upatikanaji wa fedha za ziada ambapo awali Benki ya Exim ilitaka atafutwe mfadhili mwengine kwa kiasi hichi lakini baada ya mashauriano ya muda mrefu baina ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja  na Serikali ya Watu wa China hatimae walikubaliana kudhamini kwa mkopo wa kibiashara .

Alifahamisha kuwa kutokana  na jitihada kubwa za  Serikali na Rais wa Zanzibar  Dkt Ali Mohamed Shein Benki ya Exim ilikubali kudhamini mkopo wote wa kugharamia ujenzi huo kwa utaratibu wa mkopo nafuu.

“Benki ya Exim kwa sasa imekubali kudhamini gharama zote za dola 128.7 million kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwa masharti ya  mkopo nafuu .“alisema Waziri .

Alifafanua kuwa tayari wiki hii Benki hiyo imeshamlipa mkandarasi madai yake ya dola 17.6 millioni kwa kazi ambazo ameshazifanya awali na kuidhinishwa na mshauri dola nyengine 17.6 millioni kwa kazi kama hizo lakini zenye dhamana mpya ya mkandarasi na tayari mkandarasi amelipwa jumla ya dola 35.2 millioni .

Nae Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji  Balozi Ali  Karume (pichani) alisema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kufanikiwa kwa wakati uliopangwa kwa muda wa miezi 18 hadi 20.

Aidha alisema Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano itahakikisha inasimamia vizuri ujenzi huo na kuhakikisha inatatua matatizo madogo madogo yatakayojitokeza ili  lengo la serikali la kuhakikisha jengo hilo jipya la abiria linauwezo wa kuchukua abiria 1,
200,000 mpaka 1,600,00 kwa mwaka .

Hata hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kuwashukuru Wananchi wa eneo la Chukwani   kwa ustahamilivu wao na imani yao kwa muda wote wakati serikali ikilitafutia ufumbuzi suala la mradi huo

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search