Aliyepandikizwa figo Muhimbili aruhusiwa...soma habari kamili na matukio360..#share
Na Mwandishi Wetu
PRISCA Mwingira aliyefanyiwa upasuaji wa kihistoria wa kupandikizwa figo
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ameruhusiwa kutoka hospitalini akiwa
na afya njema.
Prisca Mwingira akimshukuru kaka yake, Bathelomayo Mwingira kwa kumpatia figo kutokana na tatizo hilo kumsumbua katika kipindi cha mwaka mmoja.
Alifanyiwa upasuaji huo mkubwa na
wa kwanza kufanyika nchini ambapo
alipandikizwa figo Novemba 21, 2017 chini ya timu ya wataalam wa MNH kwa
kushirikiana na watalaam wa Hospitali ya BLK ya nchini India.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo baada ya kuruhusiwa kutoka Prisca amewashukuru watalaam wote
walioshiriki katika kumuhudumia.
Pia ametumia fursa huyo kumuomba Rais John Magufulu kuendelea kuisaidia
MNH ili kuhakikisha huduma za kibingwa zinaendelea kutolewa katika hospitali hiyo.
“Kipekee namshukuru mwenyezi
Mungu, madaktari, wauguzi, uongozi wa MNH pamoja na serikali kwa
kufanisha matibabu yangu, nilisumbuliwa na ugonjwa wa figo takribani mwaka
mzima na kuingia katika matibabu ya kuchuja damu, lakini hatimaye leo kaka
yangu amejitolea figo yake moja na nimewekewa mimi kwa kweli namshukuru sana,”.
“Napenda kuwashauri wagonjwa
wenye matatizo ya figo na wanaoendelea na huduma ya kuchuja damu wasikake tamaa
kwani sasa matibabu yamepatikana na mimi ni shuhuda katika hili,’’ amesema.
Kwa upande wake, Bathelomayo
Mwingira ambaye amemtolea figo dada yake, amefurahi kwa kusaidia kufanikisha
matibabu ya dada yake na kumuomba Mungu aendelee kuimarisha afya ya dada
yake.
Baba mdogo wa Prisca ,
Ainhard Mwingira ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kufanikisha huduma
za kibingwa kutolewa Muhimbili.
Daktari Bingwa wa Magonjwa
ya figo, Dk. Jackline Shoo wa Muhimbili amesema upasuaji wa kupandikiza figo
ulitumia takribani saa nne na zoezi hilo limekamilika vizuri na mgonjwa
anarejea nyumbani huku afya yake ikiwa salama.
“Mgonjwa anaondoka hospitalini
akiwa mzima salama kabisa,anaenda kujumuika na familia yake ataishi kama
binadamu wengine ingawa kuna masharti atatakiwa kuyafuata kama alivyoshauriwa
na wataalam,” amesema Dk. Shoo.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na huduma kwa wateja, Aminiel Aligaesha amesema upasuaji huo
umegharimu milioni 21 na endapo mgonjwa angepelekwa nchini India
matibabu yake yangegharimu milioni 80 hadi milioni 100.
“Kwa niaba ya uongozi wa MNH nawapongeza
watalaam wote walioshiriki katika upasuaji huu mkubwa na wa kihistoria na pia
naishukuru serikali kwa kufanikisha zoezi hili,’’ amesema.
No comments:
Post a Comment