Kesi Madabida mabishano ya kisheria yatawala…soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu kesho inatarajia kutoa uamuzi
katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa
Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano kama ina mamlaka ya
kuisikiliza ama la.
Aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida (kushoto).
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na hakimu mkazi mwandamizi,
Victoria Nongwa.
Ni baada ya kusikilizwa hoja zilizowasilishwa na upande wa
Mawakili wa serikali, Pius Hilla na Shedrack Kimaro na Mawakili wa utetezi,
Denis Msafiri,Makaki Masatu na Nehemia Nkoko.
Wakili wa Serikali Kimaro akiwasilisha hoja alidai kuwa
hoja ya Mawakili wa utetezi kuwa mahakama ya Kisutu inamamlaka ya
kuisikiliza kesi hiyo kwa sababu ipo chini ya bilioni 1 siyo sahihi.
Alidai kuwa ni dhahili kuwa makosa hayo ni ya uhujumu uchumi na
mamlaka yenye mamlaka ya Kuisikiliza ni Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na
Uhujumu Uchumi maarufu mahakama ya Mafisadi.
Hivyo mahakama za chini kama Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya
kuisikiliza kesi hiyo labda kuwepo na kibali cha kulipa mamlaka ya kuisikiliza
kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hivyo aliomba mahakama kutupilia mbali hoja za upande wa
utetezi.
Wakili wa utetezi, Msafiri alidai kuwa ameusikia upande wa
mashtaka, Ila ni rai yao kuwa marekebisho ya sheria ya uhujumu uchumi ya 2016
yanaipa moja kwa moja mahakama ya Kisutu kuisikiliza kesi hiyo.
Alidai kuwa kosa lolote lililopo chini ya Sh 1 bilioni haliwezi
kusikilizwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi ni Mahakama za
chini ikiwamo Mahakama ya Kisutu.
Alisisitiza kuwa mahakama ya Kisutu inamamlaka kamili ya
kuisikiliza kesi hiyo kwa vile shtaka halizidi Sh 1 bilioni na kwamba mahakama
hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo na siyo Mahakama Kuu.
Pia alidai kuwa kibali cha DPP cha kuipa mamlaka mahakama
kusikiliza kesi kinapaswa kipelekwe mahakamani pamoja na hati ya mashtaka.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Leo ambapo mahakama itatoa uamuzi na
washtakiwa waliamuliwa wapelekwe polisi.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali,Pius Hilla aliomba wapelekwe
magereza kwa sababu washtakiwa hao kuendelea kuwa mikononi mwa polisi
kuna suala la gharama na polisi hawana fungu.
Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili Nkoko aliomba mahakama
kusimamia amri yake kama ilivyoitoa.
Wakili Masatu naye aliiomba mahakama iendelee na oda yake
ilivyoitoa jana.
Hakimu Nongwa alisema suala la gharama hawawezi kulikwepa pale
Haki inapotafutwa na kuamuru washtakiwa wapelekwe polisi hadi Leo atakapotoa
uamuzi kama mahakama hiyo ina mamlaka ama la.
Madabida na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya
uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza virusi vya Ukimwi
' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.




No comments:
Post a Comment