Tanroads, wadau watakiwa kusimamia sheria...soma habari kamili na matukio360...#share

Na mwandishi wetu

Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), na Watendaji wa Mamlaka mbalimbali nchini wametakiwa kusimamia sheria ili kuhakikisha kuwa wanadhibiti changamoto za uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), kuhusu kazi zilizobaki katika barabara ya Dodoma-Mayamaya-Mela-Bonga (Babati), yenye urefu wa KM 231.5, wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo iliyokamilika kwa asilimia 98.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,  wakati akikagua barabara ya Dodoma-Mayamaya-Mela-Bonga (Babati), KM 231.5 ambapo amesema kuwa mamlaka zote hizo  zikishirikiana kwa pamoja katika suala zima la ulinzi na utekelezaji wa sheria kutasaidia miundombinu hiyo kudumu kwa muda mrefu.

"Vitendo kama vya umwagaji wa mafuta ya magari kwenye barabara, kupiga jeki, kuswaga wanyama, kuchimba kokoto na mchanga kwenye madaraja  vinachangia sana uharibifu  wa barabara, hivyo  simamieni kuhakikisha vitendo hivi vinakoma mara moja", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

 Aidha, Profesa Mbarawa,amewataka madereva kufuata alama za kudhibiti mwendo (spidi) zilizoko barabarani hususani katika kipindi hiki cha sikukuu kwani kutokufuata sheria hiyo kunapelekea  ajali nyingi za barabarani.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa ameipongeza TANROADS na Kampuni ya Mkandarasi ya CHICO kwa kuhakikisha kuwa barabara hiyo na daraja kubwa la Kelema lenye urefu wa mita 205 lililopo kwenye barabara hiyo linakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

 Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu,  amesema kuwa barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 98 ambapo  kazi zinazofanyika sasa ni uwekaji wa kingo na alama za barabarani hivyo  amefafanua kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Barabara ya Dodoma-Mayamaya-Mela-Bonga (Babati), yenye urefu wa kilometa 231.5 ambayo imejengwa kwa takribani shilingi Bilioni  257.6 inatarajiwa kufunguliwa mwakani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search