TIA, MUST wachukua ubingwa mashindano vyuo...soma habari kamili na matukio360...#share

Yusta Nkwelengushe,Mbeya
Timu ya Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) (Wanaume) na timu ya Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST)(wanawake) zimefanikiwa kuchukua ubingwa wa michuano ya vyuo yaliyokuwa yakiendelea mkoani hapa .
Timu ya soka ya wanaume ya TIA
Michuano hiyo iliyoshirikisha vyuo nane vilivyopo Mkoa wa Mbeya ilimaliza juzi kwenye Uwanja wa Chuo cha Teofilo Kisanji University(Teku) ambapo ilishuhudiwa TIA wakiichapa Chuo cha Mtakatifu Agustino (Saut) kwa bao 1-0 ,bao lililofungwa na mshambuliaji Felisian Tonelo dakika ya 19.
Mpambano mwingine ulikuwa ni upande wa Netiboli ambao uliwakutanisha timu ya Must na Saut ambapo Must waliibuka na ushindi wa mabao 17-9 na kufanikiwa kunyakua kombe la Dream Intercollege lililoandaliwa na redio Dream ya jijini hapa.
Katika michuano hiyo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa timu ambapo mshindi wa kwanza alipata Sh300,000 na kombe huku washiriki timu zingine zikipewa vyeti vya ushiriki wa michuano hiyo mwaka 2017.
Waziri wa Michezo kutoka Saut, Mwegane Yeya alisema walijipanga kuchukua ubingwa wa michuano hiyo lakini dakika 90 ziliamua mshindi na bahati ilikuwa kwa majirani zao TIA.
‘’Ni mwaka wa tatu tunafikia hatua hii ya fainali lakini hatujawahi kuchukua ubingwa ila hatukati tamaa,mwakani tutashiriki tena huenda bahati ikawa upande wetu tukanyakua ubingwa huu,’’alisema Yeya .
Yeya ambaye alinyakua zawadi ya mchezaji mwenye nidhamu alisema mchezo wa soka una matokeo matatu hivyo waliyakubali matokeo hayo.
Naye nahodha wa timu ya TIA, Ibrahimu Daudi alisema walijipanga kunyakua ubingwa huo na watahakikisha wanajinoa ipasavyo ili mwakani waweze kutetea kombe hilo.
No comments:
Post a Comment