Polisi watoa onyo waliotoka kwa msamaha wa rais...soma habari kamili na matukio360....#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeto onyo kali kwa waliotoka gerezani kwa msamaha wa rais ambao hawataki kubadilika kitabia na kifikra ili kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam SACP Lazaro Mambosasa, akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Onyo hilo limetolewa leo jijini hapa na Kamanda wa Polisi kanda hiyo SACP Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari, amesema hatua hiyo inakuja baada  kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili  wakiwa na silaha aina ya AK 47 yenye namba UC 49331998 ambayo haikuwa na magazine yake.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Ally Makwaya (40) mkazi wa Tandale kwa Tumbo na Fredrick Odhiambo (50) mkazi wa Tandale kwa Tumbo.

Katika mahojiano kuhusu wapi waliipata silaha hiyo walieleza kuwa shughuli zao kubwa ni kuokota makopo na vyuma chakavu na kuwa hata silaha hiyo waliiokota huko eneo la karakana (garage) Kinondoni Mwinyijuma.

“Natoa onyo kali kwa mtu yeyote ambaye amepata msamaha badala ya kumshukuru Mungu akabadili tabia, kubadilika kifikra, akaanza kuishi kwa kufuata sheria za nchi, anarudi kwenda kufukua silaha mahali alipoificha kwa ajili ya kuendeleza vitendo vya kihalifu niwaambie hawatabaki salama tutawakamata na  tutawarudisha huko walikotoka,” amesema SACP Mambosasa.

“Taarifa tulizonazo baadhi ya wahalifu wachache walioachiwa kwa msamaha wa rais ambao hawataki kubadili tabia zao wamekwenda sasa kufichua silaha ambazo walizizika ardhini na wanaziibua kwa ajili ya kuanza kuzitumia,” ameongeza.

Ameeleza, wengine wanashirikiana na wenzao ambao bado wako jela kwa kuwatuma mahali walipozificha silaha na kuingia nazo mtaani.

Amesema kuwa mtu akipata msamaha kitu cha kwanza anachotakiwa kufanya ni kumshukuru Mungu na kubadilika ili kufanya matendo ambayo hayavunji sheria za nchi.
Kwa mwingine jeshi hilo linawashikilia watu nane kwa makosa mbali mbali ya uhalifu.
SACP Mambosasa amesema miongoni mwa watuhumiwa hao wawili walikamatwa Januari 3, 2018 majira ya 03:30 maeneo ya Sinza karibu na kituo cha kuuza mafuta cha Big Bon na waliokamatwa ni Abdulkareem Bashir (24) na Emmanuel John Bundala (22) mwanafunzi wa Veta mwaka wa tatu kwa kujihusisha na matukio ya wizi wa magari,vifaa vya magari na wizi katika benki kwa kutumia “Master Cards na Master Keys”.

Katika tukio lingine, amesema watuhumiwa sita walikamatwa wakiwa na vielelezo mbalimbali, television nane (8), Subwoofer 1 ya Samsung na spika nne vilivyokuwa vimefichwa nyumbani kwa mtuhumiwa mmojawapo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search