Scorpion jela miaka saba kulipa fidia milioni 30...soma habari kamili na matukio360....#share
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemuhukumu Mwalimu wa sanaa ya kujihami, 'Martial arts' Salum Njwete maarufu kama Scorpion, kutumikia kifungo cha miaka saba jela na kulipa fidia ya Sh milioni 30 baada ya kupatikana na hatia ya kujeruhi kwa kumtoboa macho, Said Mrisho.
Mwalimu wa sanaa ya kujihami, 'Martial arts' Salum Njwete
maarufu kama Scorpion akitolewa mahakamani leo mara baada ya kukutwa na hatia
katika kesi ya kujeruhi ikiwemo kumtoboa macho kinyozi Said Mrisho lkwenye mahakama ya wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi, Flora Haule amesema upande wa mashtaka ulileta mashahidi kumi huku mshtakiwa akijitetea mwenyewe.
Amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kwa kifungu namba 225 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hakimu Haule alisema mahakama imejiridhisha kuwa mlalamikaji Said Mrisho alishambuliwa kutokana na majeraha mbalimbali kwenye mwili wake ambapo madaktari walithibitisha.
"Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kwamba mshitakiwa ndiye aliyemjeruhi mlalamikaji kwani ni kinyume na sheria kujeruhi au kumuadhibu mtu hata kama ana makosa. Ushahidi umeonesha kuwa Scorpion alikuwa anajishughulisha na ulinzi ambapo uhalifu eneo la Buguruni umepungua kwa kazi yake," alisema Hakimu Haule.
Alifafanua kuwa dhamira ya mshitakiwa ilikuwa ni kupambana na mtu aliyemdhania kuwa ni mhalifu na sio nia yake kuiba, hata hivyo hakuna shahidi aliyeeleza kama mshitakiwa aliiba.
Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Frank Tawale aliiomba mahakama kutoa adhabu inayostahiki kwa mshitakiwa kwa kuzingatia ulemavu aliosababishiwa mlalamikaji.
Tawale alidai kuwa Taifa limepoteza nguvu kazi kwa mlalamikaji kupata majanga hayo na kwamba familia inamtegemea kwani hawezi kuwajibika na ndoto zake zimefifia.
Akitoa utetezi, Wakili wa mshitakiwa hugo, Hussein Hitu aliomba mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na ni mtu mwema kwa kuwa hata ushahidi umeeleza kuwa uhalifu eneo la buguruni ulipungua.
Hitu alidai mshitakiwa anafamilia inayomtegemea hivyo iangalie adhabu itakayotoa ili mshitakiwa aendelee na shughuli nyingine.
Hata hivyo, Hakimu Haule alisema mshitakiwa atatakiwa kulipa fedha hizo kwa haraka kama fidia ya madhara yaliyopatikana kwa mlalamikaji.
Inadaiwa kuwa Septemba 6, 2016 maeneo ya Buguruni Sheli wilayani Ilala aliiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani sh. 60,000 kibangili ya mkononi n ash. 331,000 pamoja na pochi vyote thamani sh. 476,000, mali ya Mrisho.
Pia inadaiwa kabla ya wizi huo alimchoma na kisu tumboni mgongoni na machoni ili kujipatia mali hiyo.
No comments:
Post a Comment