ACT wamtaka msemaji wa serikali kuacha 'propaganda'....soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimemtaka Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abasi kuacha propaganda kwa kile walichodai kwamba anafanya upotoshaji kuwa nchi inafanya vizuri kwenye uchumi, demokrasia, utawala bora na haki za kiraia.
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Msimamizi huo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa  ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alipokuwa akitoa taarifa ya ziara za viongozi katika maeneo mbali mbali nchini pamoja na mafanikio ya chama kwa miezi miwili ya Januari na Februali 2018.

“Hizi ni kauli za kejeli, huwezi ukasema kwa mfano Tanzania imeimarika katika utawala bora, kila mmoja anafahamu leo ni mwathirika mara dufu katika utawala wa awamu ya tano kwenye suala la haki za kiraia, haki za binadamu na utawala bora na demokrasia,” amesema Shaibu.

Amedai msemaji huyo amekuwa akinukuu takwimu mbali mbali za ndani na nje nchi kuhalalisha hoja zake ambazo kama ACT-Wazalendo wameona kuwa ni propaganda.

Shaibu amesema amekuwa akitoa taarifa za ripoti bila kuzisoma kwa undani na kuelezea kwa uhalisia kilichoandikwa kuhusu hali ya nchi kwa mwaka huu na ilivyokuwa kwa miaka iliyopita.

“Kwa mfano ukisoma ripoti ya democracy Index inaonesha kwamba ukilinganisha mwaka 2017 na 2016 ni tofauti tumeshuka, 2016 ripoti inaonesha tulipata alama 5.76 wakati 2017 tumepata alama 5.47 huko ni kushuka, msemaji hawezi kusema haya,” ameongeza.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka jana 2017 inaonyesha Tanzania kudondoka zaidi kwenye eneo la haki za kiraia kutoka alama 5 kwa mwaka 2016 hadi alama 4.7 mwaka 2017.

Amebeinisha kwamba kumekuwepo kwa kushuka kwenye eneo la utawala bora, demokrasia na haki za binadamu ambapo amesema ripoti ya uwazi katika bujeti (Open Budget Index inayotolewa na Taasisi ya International Budget Partnership (IBP) inaonesha Tanzania imeporomoka kwa kasi kwenye eneo la uwazi kwenye bajeti kwa kupata alama 10 mwaka 2017 ukilinganisha na alama 46 za mwaka 2016.

Amemtaka msemaji wa serikali aache tabia ya kuchukua taarifa vipande vipande na kuziweka kwa umma.

Akizungumzia kuhusu ziara za viongozi wao, Shaibu amesema kuwa Februari 14, 2018 hadi Februari 25, 2018 Mwenyekiti wa chama Yeremia Maganja atafanya ziara kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga, Arusha na Kilimanjaro. Ataambatana na Mohammed Massanga, Katibu wa kapeni na chaguzi.

Amesema Makamu mwenyekiti Shaaban Mambo akiambatana na naibu katibu mkuu Bara Msafiri Mtemelwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ado Shaibu watafanya ziara kwenye mikoa ya Dodoma, Singida, Geita, Simiyu na Kagera kuanzia Februari 14, 2018 hadi Februari 23, 2018.

Katika mafanikio amesema kwa mwaka huu wamejiwekea vipaumbele vinne ambavyo ni kuimarisha muundo wa chama kupitia chaguzi, kuimarisha ushirikiano na vyama ya wafanyakazi, kuimarisha ushirikiano na vyama vingine vya siasa na kuendelea kushawishi sera za uchumi zinazomkomboa mwananchi.

Kwenye vipaumbele hivyo wamefanikiwa mambo mawili kupitia mwakilishi wao bungeni Zitto Kabwe kwa kushirikiana na wabunge wenzake. Mambo hayo kuondolewa kwa kodi kwenye mafao ya wastaafu na Fao la matibabu kwa wanachama wa NSSF.






















































About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search