CCM waituhumu Chadema.....soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam

CHAMA cha CCM kimedai kuhujumiwa na chama cha Chadema kwa vijana wake kutekwa, kupigwa, kuumizwa na wanachadema

Pia kimetuhumu kuwa Chadema kimeleta watu kutoka mikoani ili  kuharibu uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni.

Katibu wa Itikazi na Uenezi wa Chama cha Panduzi (CCM) Humphrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa uchaguzi mdogo wa marudio ya ubunge katika majimbo ya Siha, Kinondoni na udiwani katika kata 10.

“Tunazo taarifa za Chadema kuwaleta watu kutoka mikoani kwa kigezo cha kulinda kura, zipo nyumba kadhaa zimewahifadhi, tumeshatoa taarifa kwa jeshi la polisi juu ya watu hawa, hivyo ni kazi ya polisi kufuatilia na kuchukua hatua,” amesema Polepole.

Polepole amesema kura hazilindwi na kila mtu bali kuna utaratibu uliowekwa na Tume ya Uchaguzi nchini (NEC) ya namna ya kuzilinda na wahusika ni mawakala wa  vyama walioteuliwa kuwakilisha.

Akizungumzia kuhusu hujuma za Chadema dhidi yao, amedai kuwa Mwananyamala kuna kijana wa CCM alipigwa na kuchomwa bisibisi mgongoni.


Pamoja na kutoa taarifa polisi amedai kuwa wanachadema hawakukoma, waliwateka na kuwaficha vijana wa kike wa CCM ndipo kwa kushirikiana na jeshi la polisi waliwafuatilia na kuwakamata.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa  katika jimbo la Siha na kinondoni amejinasibu CCM itashinda kwa kishindo na kwa zaidi ya asilimia 50.

Amesema uhakika huo ni kutokana na kwamba chama hicho kina mtaji wa wanachama milioni 12 nchi nzima kati ya wapiga kura milioni 25 hivyo kutokana na takwimu hizo wanauhakika kushinda pasipo hata kupiga kampeni.

Amedai kinachosubiriwa ni kuwapongeza washindi na kufanya sherehe na kwamba hiyo ni ishara kwamba chama kitashinda pia kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Ameliomba jeshi la polisi kuhakikisha kunakuwepo na usalama, amani na utulivu siku ya uchaguzi ili wananchi wajitokezi na kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wao.

Katika hatua nyingine Polepole amesema yupo mbunge mmoja wa Chadema  jijini Dar es Salaam ambaye mara kadhaa amekuwa akiomba kujiunga na CCM lakini wamemkatalia.

“Yupo kiongozi mmoja hapa Dar es Salaam wa Chadema, ameomba sana tumemkataa ni gunia la michongoma, tumemkataa yeye anajua,” ameeleza.

Amedai kiongozi huyo hajafanya lolote la kimaendeleo katika jimbo lake hadi sasa na kwamba ameshamwambia 2020 atafute kazi nyingine ya kufanya kwani hatashinda.

Pia Polepole amedai  wapo wabunge wanne na madiwani wa jijini Dar es salaam kutoka vyama vya upinzani ambao wanasubiri kuwapokea 


Amesema sababu ya wabunge na madiwani hao kutaka kujiunga na CCM ni kutokana na kukubali kazi inayofanywa na serikali na kuungwa na wananchi.

Amesema kutokana na kazi kukubalika na wananchi wameona  wakiendelea kukaa upinzani 2020 hawatarudi katika nafasi zao.




About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search