MBARAWA:Fungeni kamera kuthibiti hujuma na mapato...soma habari kamili na matukio360....#share
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka kampuni ya Huduma za Meli (MSCL)
kuhakikisha inafunga kamera katika maeneo mbalimbali ya ukaguzi ili kudhibiti
vitendo vya hujuma katika mifumo ya kampuni hiyo hususani kwenye Mapato.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati) akikata
utepe kuashiria uzinduzi wa mfumo wa ukatishaji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki
katika Meli ya MV. Clarias inayotoa huduma kati ya Mwanza na Ukerewe.
Ametoa rai hiyo jijini Mwanza mara
baada ya kuzindua mfumo mpya wa ukatishaji tiketi kwa njia ya kielektroniki katika
Meli ya MV Clarias na kusisitiza kuwa matumizi ya mfumo huo mpya yaende
sambamba na elimu stahiki kwa watumishi wanaoutumia mfumo huo katika kukatisha
tiketi.
“Niwapongeze sana kwa hatua hii ya
kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki katika utoaji huduma lakini niwatake sasa
kuongeza kamera kwenye maeneo yote unapofanyika ukaguzi ili kudhibiti mianya
yote inayoweza kujitokeza ya kuhujumu mapato ya kampuni” amesema Prof.
Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea
kuwekeza kwenye shirika hilo ili liweze kupata faida na liweze kujitegemea na
kuagiza kuwa kwa sasa kila fedha inayopatikana itumike vizuri sababu Shirika
limeanza kupata faida.
Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA), kutengeneza mfumo kama huo
kwa ajili ya Shirika la Reli Nchini (TRL), ili kudhibiti uvujaji wa
mapato.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Serikali Mtandao, Dkt. Jabir Kuwe, amesema mfumo huo umetengenezwa na
Wakala ili kuiwezesha taasisi hiyo kuthibiti mapato kwani mfumo huo
utarahisisha Huduma kwani abiria ataweza kukata tiketi akiwa sehemu yoyote
nchini.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL, Bw.
Erick Hamis, amesema mfumo wa kielektroniki umeanza kwa meli moja ya MV Clarias
inayofanya Safari zake kutoka Mwanza kuelekea kisiwa cha Ukerewe ambapo katika
mpango wa baadae Kampuni inategemea kutumia mfumo huo kwenye meli zote za kampuni
hiyo.
“Toka tuanze kutumia mfumo kumekuwa
na ongezeko la mapato kwa zaidi ya asilimia 20, pia na kwenye matumizi ya
mafuta hii inatupa ishara kuwa mfumo huu utatusaidia kidhibiti mapato mengi
yaliyokuwa yakipotea kwenye tiketi”amesema Hamissi.
Ameongeza kuwa kampuni imejiwekea
mpango wa miaka miwili wa kukarabati meli Tisa za kampuni hiyo ambapo mpaka
sasa meli Tatu zimeshakarabatiwa na kuanza kazi wakati hatua ya kuanza
ukarabati kwa meli zilizobaki uko kwenye hatua mbalimbali za manunuzi.
Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa
ukatishaji tiketi katika kampuni hiyo umegharimu kiasi cha shilingi takriban
milioni 50.
No comments:
Post a Comment