Madabida, wenzake kusomewa mashtaka ya awali mwezi Machi....soma habari kamili na matukio360....#share
Na mwandishi wetu, Dar es salaam
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 16,2018 itamsomea maelezo ya awali (PH) aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na wenzake watano.
Madabida akiwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu
Maelezo hayo ya awali yanatarajiwa kusomwa siku hiyo na Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro mbele ya Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa.
Madabida na wenzake wanakabiliwa na mashtaka mawili ni ya kusambaza dawa bandia za kufubaza makali ya Ukimwi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, uzembe wa kuzuia kosa kutendeka na kusababisha hasara.
Mbali na Madabida ambaye ni afisa mtendaji mkuu, washtakiwa wengine ni Seif Shamte ambaye ni mkurugenzi wa uendeshaji, Simon Msoffe meneja masoko na Fatma Shango mhasibu msaidizi wote wa Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd. Pamoja na Sadick Materu na Evans Mwemezi ambao ni maofisa wa Bohari Kuu ya Dawa.
Madabida, Seif, Simon na Fatma wanadaiwa kuwa Aprili 5, 2011 jijini Dar es Salaam waliisambazia Bohari Kuu makopo 7776 ya dawa bandia za ARV’s zenye mchanganyiko wa dawa ya stavudin 30mg +nevirapine 200mg+lamivudine 150mg.
Dawa hizo zilizotengenezwa Machi 2011 na kuisha muda wake wa matumizi Februari 2013 huku zikionyesha kuwa ni halali wakati si kweli.Washtakiwa hao wanadaiwa pia kuisambazia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kopo 4476 .
Wanaaendelea kudaiwa kuwa walijipatia Dola za Marekani 98,506.08 ambazo ni sawa na Sh 148,350,156 za Tanzania kwa udanganyifu baada ya kuonyesha kwamba fedha hizo ni malipo ya jumla ya makopo 12252 ya dawa hizo za ARV’s.
Kwa upande wa Washtakiwa Sadick Materu na Evans Mwemezi wao wanadaiwa kuwa kati ya Aprili 5 na 13 mwaka 2011 wakiwa maafisa wa Bohari Kuu ya Dawa walishindwa kuzuia kosa kutendekea.
Washtakiwa hao wote, wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kutimiza wajibu na kuisababishia MSD hasara ya Sh 148,350,156.48 kwa kusambaza dawa hizo bandia za kufubaza makali ya Ukimwi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa hao walikana na wapo nje kwa dhamana
About Author Matukio360
Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.
No comments:
Post a Comment