MAJALIWA: Watendaji, wakuu wa idara nendeni vijijini...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watendaji na wakuu wa idara mbalimbali kuhakikisha wanatenga muda na kwenda vijijini kuwahudumia wananchi.

Amesema wananchi hususani waishio maeneo ya vijijini wanachangamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi na watendaji hao.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa mmiliki wa kiwanda kidogo cha Dotto Posho Mill, Alexander Dotto (kushoto) kuhusu unga na Mchele unaozalishwa na kiwanda hicho kilichopo eneo la Bukara, Sengerema Februari 15, 2018. Kulia ni mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyasema hayo jana (Alhamisi, Februari 15, 2018) alipozungumza kwa nyakati tofauti na watumishi na wananchi katika kata ya Nyehunge na Ibisabageni wilayani Sengerema akiwa katika ziara ya mkoa wa Mwanza.

Alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwatumikia kwa lengo la kuwaondolea kero mbalimbali zinazowakabili, hivyo hakuna sababu ya watendaji kukaa maofisini.“Watumishi wanawajibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao hasa vijijini kwa sababu si kila mwananchi anauwezo wa kufuata huduma katika ofisi zenu na atakayeshindwa kufanya hivyo hatutomvumilia.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali inawawezesha watumishi wake kwa kuwapatia vitendea kazi kama usafiri ili waweze kuwahudumia wananchi ipasavyo.Alisema kwa sababu ya kutotekeleza wajibu wao ipasavyo kumekuwa na kero na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na hivyo kusababisha wananchi kuwasilisha kero na malalamiko hayo wakati wa ziara za viongozi wakuu.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwataka wananchi wanaofanya kazi katika kiwanda cha kuongeza thamani ya mazao ya nafaka cha Doto Alex Posho Meel kuwa waaminifu.Waziri Mkuu alisema wafanyakazi hao wanatakiwa wawe waaminifu na wafanye kazi kwa bidii ili kukiwezesha kiwanda hicho kuendelea na uzalishaji.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search