Polisi kumchunguza Freeman Mbowe...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Abraham Ntambara,
Dar es Salaam
JESHI la Polisi Mkoa wa
Kipolisi Kinondoni limesema litamchunguza mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuhusu kalituhumu jeshi hilo kuhusika na mashambulizi dhidi
ya viongozi chama hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ACP Muliro Muliro, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Jana Mbowe alitoa shutuma za kutekwa, kuuwawa na watu
wasiojulikana kwa katibu wa Chadema Kata ya Hananasifu jimbo la Kinondoni, Daniel
John na mwili wake kutupwa kando ya fukwe za Coco beach.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo ACP Muliro Muliro ametoa msimamo huo leo alipokuwa akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua kauli ya jeshi hilo kuhusu tuhuma za Mbowe.
Pia alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jinsi walivyojipanga kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni.
“…Tutachunguza kauli
yake ili kujua anazungumza kwa misingi ipi na kipi kinamsukuma kutoa kauli
hizo, hatuwezi kuacha mtu azungumze kwa hisia zake,” amesema ACP Muliro.
Amesema jeshi hilo lina
taratibu za kufanya kazi zake na kwamba haliwezi kuburuzwa na hisia za mtu na
kwamba tukio hilo wanaendelea kulifanyia uchunguzi ili kubaini waliohusika na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
ACP Muliro ameongeza
kuwa Mbowe amekuwa akitoa mara kwa mara kauli za namna hiyo na kwamba
kumekuwepo na hisia kama hizo dhidi yao lakini wanapokamilisha uchunguzi na
kubaini ukweli watu huondoa hisia hizo ambapo aliwataka wananchi kutulia na
kusubiri uchunguzi ukamilike.
Kuhusu uchaguzi wa marudi ubunge kinondoni
Amesema katika uchaguzi
huo utakaofanyika Februali 17, 2018 jeshi hilo limejipanga kuhakikisha mchakato
wote wa masuala ya uchaguzi unafanyika katika misingi ya sheria, kanuni na
taratibu za uchaguzi.
Amewataka wananchi wa
mkoa wa Kinondoni kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili waweze kutekeleza haki yao
ya kikatiba kwa kufuata sheria na taratibu watakazoelekezwa siku hiyo na
wahusika wa uchaguzi bila kuleta vurugu au wao kuwa chanzo cha vurugu.
“Jeshi halitasita
kuchukua hatua za haraka za kisheria kwa mtu yeyote au kikundi chochote chenye
nia ya kupanga vitendo vya hujuma dhidi ya uchaguzi huo au kufanya vitendo
vyovyote ambavyo ni kinyume na kanuni au sheria ya uchaguzi,” amesema.
Kuhusu kukutwa kwa mwili Coco beach.
ACP Muliro amesema jana
majira ya asubuhi jeshi hilo kupitia kituo chake cha polisi Osterbay kilipokea
taarifa kutoka kwa msamaria aliyekuwa katika shughuli zake maeneo ya fukwe za
coco beach kuwa aliona mwili wa mtu akiwa kando ya bahari ya hindi.
Amesema baada ya kupata
taarifa hiyo askari walikwenda eneo la tukio na kukuta mwili wa mtu mwenye
jinsi ya kiume anayakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35 ukiwa na
majeraha kichwani, usoni, mkononi na miguuni, yanayoashiria kuwa amepigwa na
kitu chenye ncha kali.
“Mwili huo ulichukuliwa
na kupelekwa hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo madaktari walibaini kuwa
mtu huyo tayari alikuwa amekwisha fariki, jalada la kuhusiana na kifo cha mtu
huyo lilifunguliwa na uchunguzi ulianza mara moja ili kubaini chanzo cha kifo
chake,” amesema.
Kuhusu kuvamia ofisi za chadema
Amekanusha jeshi hilo
kuvamia ofisi za Chadema Magomeni na kwamba shutuma za namna hiyo dhidi yao ni
za kifedhuli, kukejeli na kulidharirisha jeshi la polisi na kwamba walichofanya
siku hiyo walirusha mabomu manne ya machozi kutawanya kikundi cha watu zaidi ya
100 waliokuwa wakifanya maandamano.
No comments:
Post a Comment