TRL yapata hasara bilioni 5.....soma habari kamili na matukio360....#share

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRL) limepata hasara ya takribani shilingi bilioni tano katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya njia ya reli ya kati kusombwa na mafuriko katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akishiriki katika kazi za kujaza mchanga kwenye viroba vinavyotumika kama kingo za kudhibiti maji ya mto Mkondoa yasifike kwenye miundombinu ya reli katika eneo la kilosa, mkoani Morogoro.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya reli hiyo na kusema kuwa Serikali imejipanga kupata suluhisho la kudumu la uharibifu katika maeneo hayo ambapo mara kadhaa yamekuwa yakiathiriwa na mvua kutokana na mabwawa yaliyopo kujaa mchanga na hivyo kusababisha uharibifu huo.

“Serikali kwa  sasa inayafanyia kazi mapendekezo matatu yaliyowasilishwa na RAHCO ikiwemo  kuihamisha reli kwenye milima jirani,  kuihamishia eneo ambapo inajengwa reli ya kisasa ya SGR ama kujenga tuta kubwa, huku tukizingatia gharama halisi za kazi hiyo kabla ya kufanya maamuzi", amesema Prof. Mbarawa. 

Ameongeza kuwa mbali na Serikali kuja na suluhu ya muda mfupi ya kurejesha safari za treni pia amewatoa hofu wafanya biashara kwa kuwahakikishia kuwa mizigo yao iko salama na itasafirishwa kwa wakati.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Mkoa umejipanga kuhakikisha unatoa elimu kwa wananchi kwenye utunzaji wa mazingira ili kunusuru uharibifu unaotokea kutokana na shughuli za kibinadamu.

“Kama Mkoa tumejipanga kuwa kuanzia sasa Sheria zilizopo zinazokataza kulima kandokando ya mito na kando ya reli sasa zitafuatwa na  tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili miudombinu hiyo isiathirike kwa sababu ya shughuli za kibinadamu zinazofanywa kupitia kilimo",  amesisitiza Dkt. Steven Kebwe.

Ameongeza kuwa kuanzia mwakani mkoa umejipanga kutenga fedha kwa ajili ya kutumia njia za asili kulinda miundombinu hiyo kwa kupanda miti na kuotesha matete ili kulinda miundombinu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Massanja Kadogosa,  amesema kazi ya ukarabati imekamilika kwa sehemu kubwa kwani tayari treni tano za mizigo zimepita salama na kuongeza kuwa kazi zinazomaliziwa kwa sasa ni kujaza mchanga kwenye matuta ya reli hiyo na kumalizia kingo ili kuilinda reli.



About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search