Ujenzi barabara lami Kidatu-Ifakara waanza....soma habari kamili na matukio360....#share

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SERIKALI imeanza ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa km 66.9 kwa kiwango cha lami, kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya za mkoa wa Morogoro.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo (kulia), katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, mkoani Morogoro.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipokuwa akikagua maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo na amemuagiza mkandarasi wa kampuni ya Reynolds Construction kutoka Nigeria anayejenga barabara hiyo kujenga kwa viwango na kukamilisha kwa wakati.

"Mradi huu umesuburiwa kwa siku nyingi na wananchi wa wilaya hii na mkoa kiujumla, mategemeo ya Serikali ni kuwa  mradi huu utakamilika mapema mwezi Aprili, 2020 kwa kuzingatia vipengele vya mkataba na kwa viwango stahiki", amesema Prof. Mbarawa.

Amesema ujenzi katika  barabara hiyo unatarajiwa kuhusisha ujenzi wa madaraja makubwa mawili, madaraja madogo manne, makalavati makubwa na madogo 271 na unatarajiwa kudumu kwa miaka 20.

Prof Mbarawa amesisitiza Serikali itahakikisha wananchi wa mkoa huo wanapewa kipaumbele kwenye ajira mara tu kazi itakapoanza ili kuongeza kipato chao.

"Mradi umeanza na nimemuelekeza mkandarasi kuajiri afisa mwajiri ili kuhakikisha nafasi nyingi za ajira zinapatikana kwa wazawa kwani nafasi 70 walizoajiri mpaka sasa ni za mwanzo tu, ila nafasi nyingine zitaongezwa", amefafanua Prof. Mbarawa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo, ameipongeza Serikali kwa jitihada inazozifanya kuboresha miundombinu ya barabara nchini na amemuahidi Waziri Prof. Mbarawa kuwa wananchi na uongozi wa usalama wa Wilaya yake watatoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili waweze kunufaika na mradi huo mapema.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Ntenga, amesema kuwa kazi halisi itaanza mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu na watahakikisha wanamsimamia mkandarasi kwa karibu ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na viwango.

Ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 kwa kiwango cha lami unatarajiwa kujengwa kwa miezi 30 na utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 111.4 na unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union), Shirika la Misaada la Uingereza (UK aid) na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search