Waziri Mbarawa aipa TAA wiki mbili....soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa wiki mbili kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), kukusanya fedha za madeni ambayo inadai kutoka kwa watoa
huduma mbalimbali katika viwanja vyote vya ndege ili ziweze kutumika kuendeleza
miundombinu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha Ndege Mwanza, Easter
Madale (kushoto), alipokagua maendeleo ya upanuzi wa kiwanja hicho mkoani
Mwanza.
Kauli hiyo ametoa jijini Mwanza,
baada kukagua maendeleo ya upanuzi wa kiwanja cha ndege na hali ya uendeshaji katika
kiwanja hicho ambapo amebaini kuwa kuna madeni ambayo yanaweza kulipika na kuweza
kurahisisha shughuli za kiuendeshaji ikiwemo kujenga uzio ili kuongeza usalama
kiwanjani hapo.
"Nataka TAA mkusanye madeni
yote mnayodai, fedha hizi zikipatikana zinaweza kutumika kujenga uzio kwa ajili
ya kulinda usalama wa uwanja ili wananchi wasiweze kuvamia na pia usalama wa ndege
zinazoruka na kutua", amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amefafanua kuwa kama Taasisi hizi
zikikusanya madeni na watoa huduma wakalipa kodi kwa wakati kutasaida Serikali
kuboresha maendeleo ya miundombinu.
Kuhusu maendeleo ya upanuzi wa
kiwanja hicho. Prof. Mbarawa amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi ambapo kwa
sasa umefikia asilimia 60.
Ameongeza kuwa ujenzi huo
unategemewa kumalizika mwezi Julai mwaka huu na utagharimu kiasi cha shilingi
takribani bilioni 94.
Aidha amesema Serikali inaendelea
kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria mara miradi inayoendelea
kukamilika.
Naye Msimamizi wa Kiwanja hicho
ambaye ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mwanza,
Mhandisi Joseph Mwami, amesema kazi
zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ujenzi wa jengo la kuongoza ndege, eneo la
maegesho na njia za kuruka na kutua ndege
Mhandisi Mwami, amefafanua kuwa njia
ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja hicho imeongezwa urefu wa mita 500 ili
kuifanya kufikia urefu wa KM 3.5 ili kuwezesha ndege kubwa za kimataifa kuweza
kutua na kuruka katika kiwanja hicho.
Katika hatua nyingine Waziri Prof
Mbarawa amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Mwaloni-Pasiansi-Airport
yenye urefu wa KM 5.3 kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake umefikia zaidi ya
asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu na utagharimu kiasi
cha shillingi bilioni 9.5.
"Nimekagua na niwapongeze
Kampuni ya wazawa ya Nyanza Road kwa kazi nzuri mliyofanya katika ujenzi kwa
barabara hii", amesema Prof Mbarawa.
Waziri Prof.
Mbarawa ametoa wito kwa wananchi kutunza na kulinda miundombinu hiyo kwa
manufaa ya kuongeza tija na maendeleo kwao kwan inapunguza msongamano wa magari
kwa kiasi kikubwa na Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia
utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri Prof Mbarawa yuko mkoani
mwanza kwa ziara ya siku akiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miundombinu
ya sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment