Lipumba afichua siri mgogoro wa CUF...soma habari kamili na matukio360...#share


Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam


Profesa Ibrahim Lipumba amesema mgogoro unaoendelea ndani ya chama cha CUF ulianzishwa na Maalim Seif Sharif akiwa na lengo la kudhoofisha chama hicho na kuwakumbatia viongozi wa Chadema


Pai amemtuhumu katibu mkuu Maalim Seif Sharif kwa kudhoofisha chama hicho kwa maslahi yake binafsi ya kung'ang’ania kuwa rais wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Tuhuma hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CUF taifa Profesa Lipumba alipokuwa akizungumza na waandisi wa habari leo jijini Dar es Salaam juu ya maazimio ya kikao cha baraza kuu la uongozi la taifa kilichofanyika jijini humo kuanzia Machi 17 hadi 18, 2018.

" Mgogoro unaoendelea ndani ya chama ulianzishwa na Maalim Seif kwa lengo  la kudhoofisha chama na kuwakumbatia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)," amesema Lipumba na kuongeza.

 "Pia amekidhoofisha chama  kwa maslahi yake binafsi ya kung'ang’ania kuwa rais wa Zanzibar."

Akizungumzia kuhusu hali ya kisiasa ndani ya chama na nchi Prof. Lipumba amesema “Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad amekidhoofisha chama chetu, kwa kutotekeleza azimio la baraza kuu la kufungua kesi mahakama kuu ya Zanzibar kupinga kufutwa matokeo ya uchaguzi wa wakilishi na madiwani ambao walikabidhiwa hati za ushindi wa majimbo na shehia zao baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015,”

Prof. Lipumba ameseama kama kesi hizo zingefunguliwa CUF ingekuwa na wawakilishi 27 wa majimbo na nusu ya wawakilishi wote wa viti maalum, pia idadi ya wawakilishi wa kuchaguliwa na wa viti maalum wa CUF ingekuwa sawa na idadi ya wawakilishi wa CCM.

Ameongeza kwamba kwa kufunguliwa kwa kesi hizo kungefanya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar ingekuwa na mawaziri wa CUF ambapo kwa hivi sasa wamewaacha chama cha mapinduzi (CCM) peke yao ambao wanatunga sheria watakavyo wao.



Amesema pamoja na mazingira magumu waliyonayo baraza kuu limeagiza juhudi kubwa zifanyike kulinda katiba ya Zanzibar ya 2010 inayotaka kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Pia baraza limemshauri Rais John Magufuli kwa nafasi yake kujiwekea ajenda ya kuimarisha demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu, kuheshimu haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara katika hali ya amani na utulivu na uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu hali ya uchumi nchini
Mwenyekiti huyo wa CUF pamoja na kuipongeza serikali kwa juhudi zake za kukusanya mapato na kutekeleza miradi mikubwa mbalimbali ya maendeleo amesema baraza limeitaka iwe na bajeti inayotekelezeka.

Kuhusu chaguzi ndogo za marudio za serikali
Prof. Lipumba amesema baraza limesikitishwa na kuvunjwa kwa taratibu katika chaguzi hizo na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) kujirekebisha. Amesema pamoja na mapungufu makubwa katika usimamizi wa uchaguzi chama kitaendelea kushiriki katika chaguzi hizo.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search