Majaliwa aagiza ufuta uuzwe kwa mnada...soma habari kamili na matukio360...#share


Na Mwandishi Wetu, Lindi


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa ufuta katika mikoa inayolima zao hilo nchini kuuza kwa kutumia njia ya minada na si mashambani.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chikwale kata ya Mbwemkulu, Wilayani Ruangwa, Waziri Mkuu yupo Wilayani ruangwa kwenye Ziara yake ya kikazi jimboni.


Ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Nachihungo, Narungombe na Chikwale.Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi amesema ili wakulima waweze kupata tija ni vema wakauza ufuta wao kwa kupitia minada kama inavyofanyika katika zao la korosho.


“Usikubali kumuuzia mtu yeyote ufuta wako ukiwa shambani kwa sababu bei atakayonunulia ni ndogo kulinganisha na soko, naamini ufuta wote ukiuzwa katika minada mtaona faida.”

Kufuatia agizo hilo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue aandae utaratibu wa maeneo ya kukusanyia ufuta na kufanyia minada.

Amesema ufuta unaolimwa nchini ni bora na unapendwa sana duniani hivyo wasiwe na wasiwasi. Baadhi ya Mikoa inayolima ufuta kwa wingi ni Lindi, Pwani, Dodoma, Manyara, Kigoma na Singida.Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema vijiji vote visivyokuwa na umeme nchini vikiwemo vya wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa katika REA awamu ya tatu.

Amesema wananchi waendelee kuwa na subira kwa sababu tayari mkandarasi ameshaanza kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vingine vya wilaya hiyo na atafika kwenye maeneo yao.Alibainisha kuwa mkakati wa Rais Dk. John Magufuli ni kuhakikisha wananchi wote nchini waunganishiwa nishati ya umeme kwenye majumba yao, hivyo waendelee kuwa na subira na kushirikiana na Serikali yao.

Kuhusu suala la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama alisema, “Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo vijiji vyote vitapata maji”.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kote nchini kutunza vyanzo vya maji ili kuliepusha taifa kugeuka jangwa pia miradi inayoletwa na Serikali iwe endelevu


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search