Meneja Machinga Complex apandishwa kizimbani....soma habari kamili na matukio360....#share

Na mwandishi wetu, Dar es Salaam,

Taasisi  ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Meneja wa soko la wafanyabiashara wadogo la Machinga Complex lililoko jijini Dar es Salaam, Nyamsukura Masondore, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.


Akisoma hati ya mashtaka inayomkabili mshtakiwa huyo, Masondore  kwa Hakimu Mkazi Adelf Sachore, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Sophia Gura alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo tarehe tofauti kati ya Septemba 29 na Oktoba 7, 2014 akiwa mwajiriwa wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kama meneja wa jengo la biashara la Machinga Complex.

Sophia alidai   kuwa  Masondore  akiwa na jukumu la kuongoza shughuli za kila siku za jengo hilo, kwa makusudi alitumia  vibaya madaraka yake kwa kutoa eneo ambalo halijaidhinishwa kwenye jengo hilo kwa Umoja wa Wauza Mitumba.

Ilidaiwa kufanya kwake hivyo  ni kinyume na kanuni namba 12(a) na (b) za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam( Bodi ya Huduma ya Jengo hilo) na kwamba kutokana na kitendo hicho mshtakiwa huyo alijipatia faida yeye pamoja na wengine.

Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alikana  na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Hata hivyo,  wakili anayemtetea, Jamuhuri Johnson aliiomba mahakama impatie dhamana mteja wake huyo na upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi.

Hakimu Sachore alitoa masharti ya dhamana akimtaka  Masondore  kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho kutoka katika taasisi zinazotambulika kisheria ambapo pia watasaini ahadi ya Sh 5 milioni. Na kwamba barua hizo zitahakikiwa.

Kesi imeahirishwa  hadi Machi 20,2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Mpaka  tunaondoka eneo la mahakama nyakati za saa tisa mchana washtakiwa walikuwa bado hawajakamilisha masharti masharti hayo

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search