Magufuli: Ukiandamana utajuta.....soma habari kamili na matukio360...#share
Na mwandishi wetu, Geita
RAIS John Pombe Magufuli, ameonya wananchi wake wanaotaka kufanya maandamano ya amani kupinga utendaji wa serikali yake, kuwa watakabiliana na jeshi la polisi.
Rais John Magufuli
"Amesema, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatakubali kuona wananchi wakiandamana kwa kuwa kufanya hivyo, ni kurudisha nyuma maendeleo ya serikali yake."
Ametoa kauli hiyo, Machi 9, 2018 kwenye sherehe ya ufunguzi wa tawi la benki ya biashara ya CRDB, nyumbani kwake, wilayani Chato, mkoani Geita
Amesema, “wapo watu wanaogependa nchi hii, kila siku iwe na migogoro. Hawa watu wameshindwa kufanya siasa za kweli, wanataka tushinde barabarani kuandamana. Nasema hivi, waache waandamane. Wataniona.”
Ameongeza, “…kama kuna watu wamewatuma hao wanaotaka kuandamana, basi wataenda kuwasimulia vizuri kitakachowapata.”
Vile vile Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema suala la maendeleo linapigwa vita sana hivyo amewataka watanzania waunge mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ili kuweza kuimarisha uchumi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
"Niwaombe watanzania tutangulize uzalendo kwanza, mahali popote tulipo tujue hatuna baba wala mama hii ndio Tanzania yetu tukiichafua tumechafuka wote na maneno muda mwingine huwa yanaumba. Nchi yetu inakwenda vizuri sana na mtu yeyote ukifanya vizuri watu hawakupendi. Uzuri una gharama", amesema Dkt. Magufuli.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameendelea kwa kusema "tunapoweza kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kwa Trioni 7.6 hela za ndani usifikili watu wanafurahi, tunapoweza kuamua kujenga uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto rufiji (Stieglers Gorge) tunapoweza kununua ndege 6 kitu ambacho tulikishindwa ndani ya miaka 50 usifikili wengine wanafurahi.
"Maendeleo yanachangamoto na vita kubwa ni lazima watanzania mjifunze na kuangalia mbele. Tumezungumza Tanzania ya viwanda ila zipo nchi zilizolalamika eti ni kwanini sisi tuwe na viwanda vya nguo kwa maana wanataka waendelee kutupa mitumba yao.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt.John Magufuli kesho (Machi 10, 2018) anatarajia kufanya ziara ya siku moja mkoani Shinyanga, kukagua na kuzindua baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo barabara inayounganisha Tanzania na Rwanda inayoanzia katika eneo la bandari kavu ya Isaka wilayani Kahama hadi Rusahunga mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment