Serikali kutoa uamuzi ununuzi wa LUKU..... soma habari kamili na matukio360....#share


Na mwandishi wetu,Dar es salaam

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema  baada ya miezi mitatu Serikali itatoa uamuzi kama nchi iendelee kutumia mita za umeme(LUKU) zinazotengenezwa nje ya nchi au kupiga marufuku uingizaji wa mita hizo baada ya kujiridhisha  na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha  mita husika.

Dk. Medard Kalemani

Msimamo huo umetolewa na Dk Kalemani   jijini Dar es Salam Machi 23, 2018 wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme lengo  likiwa ni kujiridhisha na uwezo wa kiwanda hicho katika kukidhi mahitaji ya mita nchini.

"Serikali imeweka miezi mitatu ya matazamio ili kuona kama viwanda  vyetu ambavyo sasa ni viwili, vina uwezo wa kuzalisha mita za umeme  za kutosha na zenye ubora zitakazokidhi soko la ndani, kisha tutatoa uamuzi kuhusu uingizaji wa mita hizo nchini," alisema Dkt. Kalemani.

" Miezi kadhaa iliyopita Serikali ilitoa katazo la kuagiza nguzo za umeme na transfoma kutoka nje ya nchi, baada ya kujiridhisha kuwa uwezo wa kuzalisha vifaa hivyo tunao. Sasa katika mita hizi za umeme pia tunafanya ukaguzi ili kujiridhisha na uwezo wetu," aliongeza  Dkt Kalemani.

Alisema kuwa, uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini una faida mbalimbali ikiwemo kupungua kwa gharama za usafirishaji, mita kupatikana kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa wingi.

" Mfano gharama ya  mita moja ya njia moja ya umeme (single phase) kutoka nje ya nchi ni shilingi 150,000 na njia Tatu za umeme (three phase)  ni mpaka shilingi Laki Saba lakini mita zinazozalishwa nchini unazipata si kwa zaidi ya shilingi 120,000 kwa mita za njia moja ya umeme na haizidi shilingi  Laki Nne na Nusu kwa mita za njia Tatu za umeme," alisema.

Awali Mkurugenzi wa kiwanda hicho cha Baobab, Hashim Ibrahim, alimweleza Dkt Kalemani  kuwa kiwanda hicho kina unawezo wa kuzalisha mita 38,000 kwa mwezi na kwa mwaka wanazalisha mita 456,000.

Aliongeza kuwa, mita hizo zina faida mbalimbali ikiwemo kuwa na mfumo wenye uwezo wa kuzuia matukio ya wizi wa umeme kwa asilimia 99 na kudhibiti upotevu wa umeme.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Mauzo na Masoko wa Shirika hilo, Theodory Bayona, alisema kuwa mahitaji ya Shirika hilo ni mita 20,000 kwa mwezi ambapo kati ya hizo, takriban mita 1000 ni za njia tatu za umeme. Kiasi hicho cha mita ni ajili ya wateja wapya.

Aliongeza kuwa, mahitaji ya mita za umeme bado ni makubwa kwani kuna miradi ya usambazaji umeme bado inaendelea nchini na pia kazi ya ubadilishaji wa mita za zamani bado inaendelea.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazalishaji wa vifaa vya umeme kuzalisha vifaa vyenye ubora pamoja na kutoviuza vifaa hivyo kwa gharama ya juu kwani vinazalishwa hapahapa nchini.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search