Waziri aipa TPA miezi mitatu....soma habari kamili na matukio360...#share


Na mwandishi wetu, Mtwara

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, ametoa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), kuhakikisha inatatua changamoto zote zinazokwamisha mradi wa ujenzi wa gati mpya.

Mhandisi wa Bandari ya Mtwara, Eng. Twaha Msita(katikati), akimuonyesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), ramani ya eneo la mradi wa kuegesha mizigo ya kawaida, alipokagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa katika bandari ya Mtwara. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Karim Mattaka.


 Prof. Marawa ametoa kauli hiyo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Gati mpya inayojengwa Mkoani Mtwara kwa ubia wa kampuni mbili za Kichina za China Railways Major Bridges Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) na China Railways Construction Engineering Group (CRCEG) na kubaini mapungufu katika utekelezaji wa mradi huo.

"Hatuwezi kuendelea kuchelewesha mradi huu muhimu kwa wakazi wa Mtwara, wakati fedha zipo na mikataba imeshasainiwa, naiagiza TPA kuhakikisha kuwa inatatua changamoto hizo na kuzitafutia ufumbuzi ndani ya miezi mitatu ili mradi ukamilike kwa wakati," amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza miradi inayotekelezwa na Wakandarasi wazawa chini ya usimamizi wa TPA isimamiwe kwa kuzingatia viwango na muda uliopangwa na kuahidi kurejea baada ya miezi mitatu kukagua maendeleo ya miradi hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Karim Mattaka amemuhakikishia Prof. Mbarawa kuwa TPA itasimamia kwa karibu mradi huo na kuhakikisha mapungufu yote yanafanyiwa kazi kwa wakati.

"Nipende kukuhakikishia Waziri kuwa  TPA tumejipanga vizuri kuhakikisha tunatatua changamoto zilizopo na kuanzia wiki ijayo tutaongeza kasi ya kutatua mapungufu yaliyopo ili mradi huu ukamilike kwa wakati,"amesema Mhandisi Mattaka.

Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Nelson Mlali amesema kwa sasa mradi wa ujenzi wa gati namba mbili (2) umefikia asimilia 15 na utakapokamilika utawezesha Meli kubwa na za kisasa aina ya Panamax kuhudumiwa katika Bandari ya Mtwara ifikapo mwaka 2019.

Katika hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua ujenzi wa Barabara ya Mtwara hadi Mnivata KM 50 na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kuahidi kulipa madai ya Mkandarasi Kampuni ya M/s Dott Services ltd mapema iwezekanavyo ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

"Nimhakikishie Mkandarasi kuwa madai yake aliyowasilisha tunajipanga kuyalipa ili kasi iwe kubwa na mradi huu ukamilike kwa wakati kwa kuwa umesubiriwa na wananchi wa mkoa wa Mtwara kwa muda mrefu," amesisitiza Prof. Mbarawa.

Aidha, Mkandarsi wa Kampuni ya M/s Dott Services ltd amemhakikishia Waziri  kuwa watahakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango kama ilivyoahidiwa.

Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) , Mkoani Mtwara, Eng. Dotto John amesema wakala umejipanga kuhakikisha unasimamia barabara hiyo kwa kuhakikisha viwango na ubora vinazingatiwa na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Prof. Mbarawa yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku moja kukagua maendeleo ya miradi ya Miundombinu ya Barabara na Bandari.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search