HakiElimu yataja changamoto saba sekta ya elimu nchini…soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara,
Dar es Salaam
TAASISI ya HakiElimu
imetaja changamoto saba zinazotakiwa kushughulikiwa na serikali kwenye mpango
bajeti wa sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuiboresha sekta
hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dk. John Kalage akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Changamoto hizo ni upungufu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya
bajeti ya sekta ya elimu, upungufu wa bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu na
kutenga fedha zinazojitosheleza, kutatua changamoto za utekelezaji wa bajeti ya
maendeleo ya sekta ya elimu.
Nyingine ni kushughulikia changamoto za miundombinu
mashuleni, Bajeti kwa ajili ya ajira za walimu, bajeti kwa ajili ya ruzuku kwa
wanafunzi na bajeti kwa ajili ya elimu kwa mtoto wa kike.
Changamoto hizo zimetajwa
leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dk. John Kalage
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa muhtasari wa taarifa
ya taasisi hiyo kuhusu mpango wa bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha
2018/2019.
“…tunatambua kuwa
jitihada za serikali zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinafifisha
ubora na kudumaza juhudi za uboreshaji wa elimu nchini. Mathalani, katika miaka
ya hivi karibuni, sekta ya elimu imekabiliwa na kushuka kwa uwezo wa kusoma,
kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa elimu ya msingi wa madaraja yote (UWEZO,
2017) amesema Dk. Kalage.
“Ni asilimia 20 tu ya
wanafunzi wa darasa la nne nchini wanauwezo wa kusoma sentensi kwa ufasaha na
chini ya asilimia 10 wakiwa na uwezo wa kusoma aya kwa mujibu wa Ripoti ya
Benki ya Dunia (2018), huku matokeo ya mitihani ya mwisho kidato cha pili na
nne yakionesha ufaulu hafifu ambapo wastani wa asilimia 60 ya watahiniwa
wanapata alama za daraja la nne na sifuri,” ameongeza.
Dk. Kalage ametoa mapendekezo
yakufanywa na serikali katika bajati ya 2018/2019 ili kukabiliana na changamoto
hizo na mioungoni mwa mapendekezo hayo ni serikali
ielekeze asilimia 20 ya bajeti ya serikali kwenda katika sekta ya elimu ili
kukidhi mahitaji ya sekta na kukazia utekelezaji wa makubaliano ya kikanda na
kimataifa.
Mengine ni serikali
itenge na kuongeza bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya
elimu na hasa fedha zinazokwenda TAMISEMI kwa ajili ya elimu ya msingi. Serikali
itenge bajeti yenye uhalisia wa kutatua changamoto sugu na za muda mrefu za
miundombinu ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiathiri mazingira ya kusoma na
kufundisha katika shule za serikali.
Ameshauri serikali
kuweka kipaumbele katika suala la ajira za walimu ili kutatua tatizo hilo
endelevu linalosababisha changamoto kubwa za kujifunzia shuleni na kwa sababu
wasichana ndiyo waathirika wakuu wa mazingira na miundombinu duni ya kujifunzia
katika shule za serikali ni muhimu
masuala yanayoboresha ustawi wao kupewa kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa
fedha 2018/19.
No comments:
Post a Comment