Lissu azungumzia ujio wa Bombardier iliykuwa imezuiliwa Canada...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Singida, Tundu Lissu amesema ameona taarifa ya Msemaji
wa Ikulu, Gerson Msigwa, kwamba ndege aina Bombardier iliyokuwa imezuiliwa
Canada inakuja nchini.
Tundu Lissu
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Lissu ameandika baadhi ya
mambo ambayo angependa baadhi ya watu wanaodai kuwa alitumwa kipindi cha nyuma
alipokuwa anazungumzia kushikiliwa kwa ndege hiyo Canada wafahamu.
Jambo la kwanza alilolisema Lissu katika ukurasa wake wa
Instagrama ni kuhusu kuvunjwa kwa mkataba uliosababisha ndege kuzuiliwa “Mwaka
2003, kampuni ya Sterling Construction and Engineering Ltd. (SCEL), ilivunjiwa
mkataba wake wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo. Mkataba huo ulivunjwa na Wizara
ya Ujenzi na Uchukuzi.”
“Baada ya kuvunjwa kwa mkataba, SCEL ilishtaki Serikali ya
Tanzania kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya International Chamber of Commerce,
London. Tunaambiwa baadhi ya hearings, au zote, zilifanyikia Dar Es Salaam.”
-Lissu
Jambo la pili aliloliandika Lissu ni kuhusu serikali kuamriwa
kulipa kampuni “December 2009 na baadae June 2010, Arbitral Tribunal ya ICC
ilitoa uamuzi kwamba Serikali ya Tanzania ilivunja mkataba wa SCEL bila uhalali
wowote na kuamuru Serikali kuilipa SCEL takriban USD milioni 25, na riba ya 8%
kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hadi tarehe ya malipo ya mwisho.”
“Kwa sababu tunazostahili kuambiwa na Serikali , deni la SCEL
halikulipwa kwa miaka saba hadi SCEL walipoenda kwenye Supreme Court of Quebec,
Canada, na kupata amri ya mahakama kuikamata Bombardier.” -Lissu
Lissu akaendelea kuandika kwamba baada ya kusikia Bombardier
imekamatwa, Waziri wa Mambo ya Nje, Dr. Augustine Mahiga, na Balozi wetu
Canada, Jack Zoka, walitumwa kwenda Toronto kufanya mazungumzo na SCEL juu ya
namna ya kujinasua. Waziri Mahiga na Balozi Zoka waliiomba SCEL isitoe habari
za Bombardier kukamatwa hadharani.
“August 18, 2017, baada ya kupata nyaraka mbali mbali zinazohusu
kukamatwa kwa Bombardier, nilitoa taarifa za kukamatwa ndege hiyo kwa waandishi
wa habari Courtyard Hotel, Dar Es Salaam.” -Lissu
“August 19, Kaimu Msemaji wa Serikali, Zamaradi Kawawa,
alithibitisha kukamatwa kwa Bombardier ya Magufuli na kutulaumu sisi wapinzani
kuwa ndio tuliosababisha ndege yetu ikamatwe Canada.” -Lissu
“Licha ya Serikali kukiri ukweli wa maneno yangu, tarehe 20
August, nilikamatwa na askari polisi walioniambia hawajui kosa langu ila
wanatekeleza ‘maagizo.’ Nililazwa mahabusu hadi kesho yake nilipopelekwa kwa
Mkemia Mkuu ili kupimwa mkojo. Nilipokataa kupimwa mkojo nilirudishwa mahabusu
hadi kesho yake tarehe 22 August nilipoachiliwa huru bila kupelekwa
mahakamani.” -Lissu
“September 7, 2017, siku kumi na moja baada ya shambulio la
mabomu dhidi ya IMMA Advocates, ikawa zamu yangu kushambuliwa kwa risasi za
submachine guns na ‘watu wasiojulikana.’ Nilijeruhiwa vibaya sana, lakini Mungu
ni mwema sikufa. Hadi ninapoandika maneno haya, hakuna mtu hata mmoja
aliyetuhumiwa au kukamatwa na kushtakiwa kwa kuhusika na shambulio hilo la
kigaidi dhidi yangu.” –Lissu
Lissu akamaliza kwa kusema “Nafurahi kusikia taarifa za
kuachiliwa kwa ndege yetu. Nitafurahi zaidi tukiambiwa Bombardier hiyo
imeachiliwa kwa masharti gani, kwa vile tulikuwa tunadaiwa karibu USD milioni
40 zilizotokana na kuvunja mkataba na Serikali kushindwa kesi na SCEL. Hili ni
swali ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kuwahoji hawa watoa taarifa za
kuachiliwa kwa Bombardier.”
No comments:
Post a Comment