Majaliwa awaomba viongozi wa dini kulinda amani...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini popote
walipo wahakikishe wanaipigania na kuilinda amani kwa kila hali ikiwa ni pamoja
na kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Machi 31, 2018)
kwenye Mkutano Mkuu wa BAKWATA uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini
Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu wasaidizi wa Mufti wakasimamia suala
hilo.
“Dini ni taasisi muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku ndio
maana Serikali inaheshimu na kuzitambua dini zote kutokana na mchango wake
mkubwa katika amani ya nchi yetu. Niwaombe viongozi wangu popote mlipo muilinde
amani yetu”
Waziri Mkuu amesema amani ni miongoni mwa neema kubwa sana kwa
binadamu na ndio maana wote wanamtambua Mwenyezi Mungu, hivyo wasiruhusu mtu au
kikundi chochote kujaribu kuchafua na kuharibu amani iliyopo nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi Baraza
Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wahakikishe kuwa chombo hicho kinaendelea
kuwaunganisha waislamu bila ya kujali makabila yao, rangi zao au madhehebu yao.
Waziri Mkuu amesema Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar bin
Zubeiry ambaye ndiye kiongozi wa Waislamu nchini mara zote amekuwa akisisitiza
jambo hilo na kuwataka waislamu popote walipo watambue kuwa hicho ni chombo
chao.
“Ni muhimu sana kwa ninyi wasaidizi wa Mufti mlio kusanyika hapa
muhakikishe mnalisimamia hili katika maeneo yenu. Katika hili napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali yenu iko pamoja Mheshimiwa Mufti kutekeleza nia
hiyo njema.”
Amesema ahadi ya Rais Dkt. Magufuli ni kuwa Serikali
anayoiongoza ipo tayari kusikiliza maoni, ushauri na mapendekezo yeyote
kutoka kwa viongozi wa dini . ‘Milango iko wazi saa zote ‘
Ameongeza kuwa yeye si mtaalamu sana kama walivyo Masheikh hao
lakini anakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ani sura Al Imran aya
ya 103 yanayosema “ Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote na wala
msifarakane”
Mkutano huo umehudhuriwa na Sheikh Mkuu wa Mufti wa
Tanzania Sheikh Zubeir, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, wajumbe wa
Baraza la Ulamaa, Masheikh na viongozi wa BAKWATA wa mikoa na wilaya zote
Tanzania.
No comments:
Post a Comment