Majambazi wavamia kanisa na kupora sadaka...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAJAMBAZI wamevamia Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu
Theresia wa Mtoto Yesu-Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam na kupora fedha na
baadhi ya vifaa vya kuendeshea misa usiku wa kuamkia leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango, Uchumi na Fedha wa parokia
hiyo, Arnold Kimanganu amesema kuwa majambazi hao waliwapiga walinzi kabla ya
kuingia kanisani.
“Majambazi walivyofika waliwapiga walinzi, tuna walinzi wanne
walimshika mlinzi mwenye silaha wakampiga na kumnyang’anya bunduki, kumkamata
mwingine wakampiga na kumfunga na wakaingia sehemu inaitwa sakristia, wakavunja
milango ya sakristia wakakusanya matoleo yote yaliyokuwa yamehifadhiwa
yaliyokusanywa kipindi cha pasaka,” amesema Kimanganu.
Paroko wa parokia hiyo, Sunil Kishor amesema majambazi hao
walivamia kanisa hilo saa tisa usiku na wameiba fedha na baadhi ya vifaa vya
kuendesha misa.
“Ni kweli majambazi walivamia kanisa letu majira ya saa tisa
alfajiri, walichochukua kuna pesa za sadaka ambazo zilikuwepo sakristia, vifaa
vya misa hasa vikombe na siborio,” amesema Paroko Kishor na kuongeza kuwa;
“Kiasi cha fedha ambacho wamechukua kadri ya hesabu ni kama
milioni nane hivi, Tumesharipoti polisi na wapo hapa kanisani wanaendelea na
uchunguzi.”
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri kutokea ingawa bado hajapata taarifa
ofisini kwake kimaandishi .
‘’Ni kweli vibaka walivamia na wameiba sadaka, lakini bado
sijalipata vizuri tukio hili nikilipata nitalitolea taarifa, lakini
nathibitisha kutokea kwa tukio hilo,” amesema Kamanda Mambosasa.
No comments:
Post a Comment