Watumishi wa sekta ya ujenzi watakiwa kujitathimini...soma habari kamili na matukio360...#share

Na Mwandishi Wetu, Morogoro


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi kujitathimini yale waliyoazimia kutekeleza kwa mwaka wa Fedha 2017/18 kama yamefikia lengo ili kuweza kusaidia kuboresha utendaji na kutafutia ufumbuzi masuala ambayo yanakwamisha ufanisi wa kazi na kuwezesha mazingira wezeshi kwa wafanyakazi.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa baraza hilo lililofanyika mkoani Morogoro.

Prof. Mbarawa amesema hayo mkoani Morogoro, wakati akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi ambapo pamoja na mambo mengime amesisitiza umuhimu wa baraza hilo katika kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wenye tija, staha na upendo.

"Ni matarajio yangu kuwa kila mjumbe kwa nafasi aliyonayo katika baraza hili atatumia fursa hii kutoa michango ya mawazo ili iweze kuwa mwongozo mzuri wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi", amesema Prof. Mbarawa. 

Aidha, ametoa wito kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa Wizara inashiriki kikamilifu katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuwajengea watanzania miundombinu bora na imara ili kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na hivyo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kuifanya nchi yetu iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Profesa Mbarawa, amewataka wajumbe hao kujadili kwa kina Rasimu ya Bajeti na Mpango wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2018/19 ili kuweza kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Waziri Prof. Mbarawa, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi za Umma kuhusu usimamizi wa rasilimali watu, utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na weledi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma. 

Ameongeza majukumu mengine kuwa ni kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi; kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi; maslahi ya Wanyakazi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search