TIC yawataka watanzania kuchangamkia fursa ujio wawekezaji nchini..soma habari kamili na matukio360...#share

Na Abraham Ntambara, Dar es Salaam
KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC) kimewataka
watanzania kuchangamkia fursa ya ujio wa wawekezaji katika kujinufaisha
kiuchumi na ukuaji wa viwanda kwa kushirikiana nao kibiashara.
Bw. Geoffrey Mwambe (wa pili kutoka kulia) akiinadi Tanzania
kwenye jipo la wataalamu wa uchumi walioongoza mjadala wa upatikanaji wa
mitaji, mazingira na fursa za uwekezaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
wakati wa kongamano la Ujerumani na Afrika Masghariki, Berlin.
Hayo
yamesemwa na leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji Kituo hicho Geofrey Mwambe wakati akizungumza
na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusiana na ziara aliyofanya
ya kikazi nchini Ujerumani na Uholanzi kati ya tarehe 14 mpaka 17, Mei 2018
ikiwa ni jitihada zake za kutangaza fursa za uwekezaji ili kushawishi na kuvutia wawekezaji kuja
kuwekeza nchini.
“Ni vyema wawekezaji wa
hapa nchini wakajenga uhusiano mzuri na wawekezaji kutoka nje ya nchi kwani ni
jambo ambalo litasaidia kuendelea kukuza maendeleo ya uchumi wa viwanda,”
amesema Mwambe.
Amesema watanzania wanatakiwa
kujitokeza kwa wingi kujiunga na wawekezaji kutoka nje ili waweze kupata uelewa
wa kutosha katika ufanyaji wa biashara wa kimataifa lakini pia kufahamu mtu
ambaye wanataka kufanya naye biashara.
Mwambe amesema pamoja na
kutokuwa na mitaji ya kutosha, amewataka baadhi ya watanzania kuepukana na
dhana ya kuwa wawekezaji ni kutoka nje ya nchi pekee bali nao wanapaswa
kuwekeza kwa kutumia fursa zilizopo kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri.
Hapa chini ni taarifa kamili za Ziara ya
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geofrey Mwambe katika nchi za Ujerumani na Uholanzi.
MKURUGENZI
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. Geoffrey Mwambe amefanya
ziara ya kikazi nchini Ujerumani na Uholanzi kati ya tarehe 14 mpaka 17, Mei 2018
katika jitihada zake za kutangaza fursa za uwekezaji ili kushawishi na kuvutia wawekezaji kuja
kuwekeza nchini.
Akiwa
nchini Ujerumani Bw. Mwambe alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani
Mhe. Dkt. Possi Abdallah ambapo walifanya kikao cha kazi kabla ya kushiriki kongamano
la biashara na uwekezaji kati ya Ujerumani na nchi za Afrika Mashariki lililofanyika
Mei 15, 2018 katika mji wa Berlin. Kongamano liliandaliwa ili kutoa nafasi kwa nchi
za ukanda wa Afrika Mashariki kunadi fursa za uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Ujerumani
na dunia kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Bw. Geoffrey Mwambe (kulia)
alipomtembelea Balozi wa Tanzania nchini
Ujerumani Mhe. Dkt. Possi Abdallah ofisini kwake Berlin, Ujeruman.
Vilevile siku
mbili baada ya kongamano, Kituo kilifanya ziara nchini Uholanzi ambapo kilifanikiwa
kusaini makubaliano ya mashirikiano (MOC) na Taasisi ya Biashara za Kimataifa
ya Uholanzi (DCIB) pamoja na kufanya mkutano na baadhi ya wafanyabiashara wa
Taifa hilo wenye nia ya kuja kuwekeza nchini. Sekta zitakazohusika ni pamoja na
mafuta, gesi, kilimo, afya, usafirishaji, viwanda, fedha, mazingira, nishati na
mawasiliano.
Pichani baada ya kukamilisha zoezi la kusaini MOC . waliokaa
kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Geoffrey Mwambe na kushoto ni
Mwenyekiti wa DCIB Bw. Hans Biesheuvel. Pamoja nao kulia ni Mkurugenzi wa
Uhamasishaji Uwekezaji wa TIC Bw. John Mnali,Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi
Mhe. Irene Kasyanju,Mkurugenzi Mkuu wa DCIB Dkt Dewanand Mahadew na Bi Zeinab
Dauda Meneja wa DCIB Afrika Mashariki.
Makubaliano yaliyomo
kwenye MOC yatadumu kwa kipindi cha miaka mitano (5) na malengo yake ni:
i. I/ kubadilishana
taarifa za fursa na mazingira ya uwekezaji
ii. kuratibu
ujio wa wafanyabiashara wa Uholanzi kuja Tanzania kuwekeza na kufanya biashara na Watanzania
kwenda Uholanzi
iii. II/ kujengea
uwezo Kituo cha Uwekezaji kufanya kazi zake za kutafiti, kuhamasisha na
kufanikisha uwekezaji
iv. III/ kukuza
sekta binafasi ya Tanzania hususan wawekezaji wa ndani na wajasiriamali kupitia
mafunzo mbalimbali.
Kupitia kongamano, Bw. Mwambe alielezea
majukumu ya Kituo, msaada unaotolewa kwa wawekezaji katika kuanzisha miradi,
hali ya uchumi na mikakati mbalimbali inavyotekelezwa na Serikali ya awamu ya
tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara
na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa mitaji ya kutoka nje (FDI).
Akiainisha baadhi ya maeneo ambayo
yanafanyiwa kazi na Serikali alisema ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya usajili wa
biashara na leseni kwa wawekezaji wa ndani na nje pamoja na kuondoa urasimu
ndani ya mifumo ya Serikali kuanzia ngazi ya Mtaa/Kijiji hadi Taifa ili
kufanikisha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji kwa muda mfupi.
Bw. Mwambe pia aliwahakikishia wawekezaji
wa nchini Ujerumani na Dunia kwa ujumla kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa
nyingi na mahali salama kwa uwekezaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Afrika; hivyo wawekezaji wenye mitaji na
teknolojia wanakaribishwa kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ambazo kwa sasa ni kipaumbele cha Taifa yaani
viwanda, kilimo, madini, mifugo, uvuvi, miundombinu, uzalishaji na usambazaji
umeme na miundombinu kwa ujumla.
Nae mwakilishi
wa Benki ya Stanbic kwa Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Jibran Qureishi alieleza
kuwa kwa sasa Tanzania inafanya vizuri katika masuala ya Kiuchumi ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Matokeo hayo chanya ni kutokana
na uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyeanzisha vita
ya kupambana na rushwa; na kupunguza urasimu kwa lengo la kuweka mazingira
wezeshi ya uwekezaji.
Sehemu ya washiriki wa kongamano la
Biashara na Uwekezani kati ya Ujerumani na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
wakifuatilia mawasilisho ya mada ya juu ya hali ya uchumi kwa nchi za Afrika
Mashariki
Bw. Qureishi
ambaye ni mchumi mbobezi aliweka bayana kwamba Tanzania ina nafasi kubwa ya
kuendelea kufanya vizuri zaidi katika nyanja ya uchumi kwa miaka ya hivi
karibuni baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwa kutumia rasilimali za ndani na
sio mikopo kama ilivyokuwa imezoeleka.
Akitaja baadhi ya miradi hiyo ni mradi
wa kuzalisha umeme wa Stiegler's Gorge, ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es
salaam mpaka Dodoma na upanuzi wa bandari. Kwa ujumla ziara ya Kituo nchini
Ujerumani na Uholanzi imekuwa ya manufaa yenye manufaa kwenye maeneo
yafuatayo:-
Moja, kwa upande wa Ujerumani tumekutana na
makampuni ambayo yameonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta za viwanda, afya,
ujenzi, miundombinu, mawasiliano, usafirishaji na nishati.
Pili, kuanza kwa utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Kituo na Taasisi
ya Biashara za Kimataifa ya Uholanzi kunatoa fursa ya kutekelezwa masuala mbalimbali
kwenye miradi ya ubia, upatikanaji wa fedha za miradi, uhamishaji wa teknolojia
na ujuzi, kuandaa semina /warsha na misafara ya wawekezaji. Kituo kinatarajia
kupokea kundi la kwanza la wafanyabiashara kutoka Uholanzi mapema mwaka
2018/2019.
Tatu, kwa upande wa Uholanzi tumekutana na
makampuni yaliyoonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta za utalii, ujenzi wa
kiwanda cha kutengeneza spea za magari, uanzishaji wa chuo cha mafunzo ya
ufundi (Vocational Training), uanzishaji wa mradi wa usimamizi wa usalama wa
mizigo kuanzia bandarini mpaka eneo husika na usimikaji wa mitambo ya
kutengeneza bidhaa mbalimbali za ngano.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TIC Bw. Geoffrey Mwambe alipomtembelea Balozi wa Tanzania nchini
Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju ofisini ,The Hague, Uholanzi.
Kwa upande wake
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju amesema kusainiwa kwa
makubaliano kati ya TIC na DCIB ni hatua kubwa ambayo itarahisisha utekelezaji
wa sera, diplomasia ya uchumi. Mhe. Balozi amehitimisha kwa kuhimiza wadau wa
sekta binafsi ya Tanzania kutumia vema makubaliano hayo kama fursa ya kuongeza
biashara na uwekezaji kwa kushirikiana na wadau kutoka Uholanzi.
No comments:
Post a Comment