UDART yataja sababu abiria mabasi mwendokasi kusafiri bure...soma habari kamili na matukio360...#share
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI inayotoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART) imesema sababu kubwa iliyosababisha kutoa huduma kwa abiria kwenye mfumo wa bila ya kulipa nauli kwa siku mbili mfululizo ni kutokana na wahudumu wanaouza tiketi kugoma kufanya kazi.
Abiria wa mabasi hayo wamekuwa wakipata huduma ya usafiri bila malipo tangu Juni 3 hadi leo Juni 4, 2018.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano UDART, Deus Bugaywa amesema wamefikia hatua hiyo kwa lengo la kutoathiri shughuli za abiria hao.
"Tunatambua kusafirisha abiria bila ya kulipa nauli kuna sababisha hasara kubwa kwa kampuni lakini kwa kuzingatia umuhimu wa abiria wetu kupata huduma na hadhi ya taifa, hasara iliyopatikana haiwezi kuzidi madhara ambayo yangetokea kwa kusimamisha huduma", amesema Bugaywa.
Pamoja na hayo, Bugaywa ameendelea kwa kusema "kutokufika kwa wahudumu kwenye vituo kwa siku mbili mfululizo kumetokana na kucheleweshewa mishahara ya mwezi Aprili na Mei ambayo awali ilikuwa inalipwa na UDART kupitia Maxcom. Lakini badala ya mkataba huo kuisha na wakati tukisubiri kamati zilizoundwa na wakala anayesimamia mradi DART Agency, kusimamia na kukabidhi mfumo kwa UDART.
Kampuni iliomba taarifa za benki za wafanyakazi hao ili waweze kulipwa mishahara moja kwa moja kutoka UDART, bahati mbaya hil halikuwezekana hadi sasa tumefikia hatua hii".
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano UDART, Deus Bugaywa amewahakikishia abiria wa mfumo huo na wananchi kwa ujumla kuwa mradi huo ni muhimu kwa ustawi wa taifa na kwa namna yeyote hawapo tayari kuhatarisha uendelevu wake kwa manufaa mapana ya taifa.
No comments:
Post a Comment