Rukwa kushirikiana na Ireland kuongeza uzalishaji wa alizeti...soma habari kamili na matukio360...#share


Na Mwandishi Wetu, Rukwa

BALOZI wa Jamhuri ya Ireland Paul Sherlock amepokea maombi ya ushirikiano baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na nchi yake yaliyolenga kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti mkoani humo jambo litakalopelekea kuinua kipato cha mkulima wa mkoa wa huo.
 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akipeana mkono na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Paul Sherlock muda mfupi baada ya maongezi ya mikakati ya kukuza uzalishaji wa zao la Alizeti Mkoani Rukwa.


Maombi hayo yaliyowasilishwa na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kwa balozi huyo mapema mwezi huu yalionyesha hali ilivyo ya uzalishaji wa zao hilo kwa sasa, ambapo kati ya hekta za shamba la Alizeti 0.5 hadi 2 huzalisha tani 1.1 badala ya tani 2.5.

“Nimefurahishwa sana na jitihada za Mh. Joachim Wangabo kwa kuona umuhimu wa kutafuta zao mbadala la biashara katika Mkoa wa Rukwa ikiwa ni pamoja na kuinua kulimo cha mkoa na kuinua kipato cha wakulima wadogo na hatimae kuwatafutia namna ya kuongeza viwanda vidogo na kuongeza ajira,” Alisema Balozi Sherlock.

Kwa upande wake Mh. Wangabo amesema kuwa zao la mahindi linazalishwa kwa wingi sana katika mkoa wake na wakulima hulichangamkia hilo zaidi ila bei ikitetereka wakulima hao wanakosa pa kujishika hivyo kwakuwa zao la alizeti ni la pili la kibiashara basi ni vyema kulitafutia mikakati liwe sawa na zao la mahindi ili wananchi wachague.

“Kwa mwaka 2016/2017 hekta 47,862 zililimwa alizeti na tukapata tani 53,470 ambayo ni chini ya kiwango tunachotakiwa kuzalisha kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa hekta 47,862 zikilimwa vizuri tunaweza kupata tani 119,655 ambayo ni ongezeko la asilimia 55, tunataka kufika huko, tuzalishe mafuta ya alizeti kwa wingi, kutengeneza ajira na kuongeza viwanda,” Alisema Mh. Wangabo.

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutalipunguzia taifa mzigo wa kununua mafuta nje ya nchi jambo linalopelekea serikali kutumia pesa nyingi kufanya manunuzi na hatimae pesa hiyo kubaki kwa wakulima wetu. 

Mkoa wa Rukwa unatarajia kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Faida mali ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukuza zao la alizeti katika Mkoa wa Singida ili kuhamishia ujuzi huo katika Mkoa wa Rukwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji, Tanzania hutumia Shilingi bilioni 189.6 kila mwaka kununua mafuta ya kula nje ya nchi huku ikizalisha tani 91,000 ambayo ni sawa na asilimia 40 za mafuta hayo tofauti na makadirio ya tani 200,000 hadi 300,000 ya uhitaji wa bidhaa hiyo kwa mwaka.


About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search