WALIMU 7000 KUHAMISHWA TOKA SEKONDARI KWENDA SHULE YA MSINGI

SERIKALI
imesema itawahamisha walimu wa ziada katika masomo ya sanaa kwenye shule za
sekondari wapatao 7,463 kwenda shule za msingi kupunguza upungufu na kuboresha
elimu hiyo ya msingi.
Aidha,
tayari majaribio ya mpango huo wa kuwahamishia walimu hao uameanza katika Mkoa
wa Arusha na yakifanikiwa, itahusisha mikoa yote nchini hasa kwenye mahitaji.
Naibu
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
Elimu, Bernard Makali alisema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) wakati kamati hiyo ilipokuwa ikichambua taarifa za Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kamati
ilikuwa inakagua taarifa hiyo kuhusu ufanisi katika Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.
Makali
alisema katika sekondari walimu wa sanaa (Arts) ni wengi kwa idadi hiyo ya
zaidi ya 7,000 na kwamba hao wanaohamishwa wanachochea ubora wa elimu katika
shule za msingi na marupurupu yao na mishahara itabaki kama ilivyo.
Kwa mujibu
wa Makali, shule za msingi nchini zina upungufu wa jumla wa walimu 47,151 na
ziada ya walimu wa sanaa katika shule za sekondari ni hiyo 7,463 na ndio
watakaopelekwa shule za msingi.
Naibu
Katibu Mkuu alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Kilindi, Omari Kigua (CCM)
alihoji kwa nini walimu wengi wa shule za msingi wanajiendeleza lakini
wakirejea kazini, wanabaki kufundisha shule hizo za msingi badala ya
kupandishwa wafundishe sekondari.
Akijibu
hoja hiyo, Naibu Katibu Mkuu alisema asilimia 90 ya walimu wa shule za msingi
wanaokwenda kujiendeleza, wanachagua masomo ya sanaa na walimu wa masomo hayo
ni wengi katika shule za sekondari kiasi kwamba wengine wanagawana mada (topic)
badala ya vipindi katika ufundishaji.
Makali
alitoa mfano wa Shule ya Sekondari ya Makole ya Dodoma ambayo ina mwalimu mmoja
wa fizikia ambaye pia ndiye mwalimu mkuu huku ikiwa na walimu wa sanaa wakiwa
na ziada.
“Tumeanza
na ‘pilot’ (majaribio) mkoani Arusha na tutafanya kwa nchi nzima ili
kujiridhisha na kuhakikisha lengo linatimia,” alifafanua Naibu Katibu Mkuu
Tamisemi.
Kuhusu
upungufu wa walimu wa hisabati na sayansi, alisema wamepata kibali cha kuajiri
walimu 4,129 wa masomo ya sayansi na wataalamu wa maabara.
Aidha,
baadhi ya wajumbe wa kamati waliuliza kuhusu kuwepo kwa walimu wasio na sifa
kazini na kutaka kujua hatua zinachukuliwa na serikali hasa baada ya kuweka
utaratibu kwao kwenda kujiendeleza.
Chanzo:
Habari leo
No comments:
Post a Comment