ALICHOONGEA KATIBU MKUU WA YANGA SC NA WAANDISHI WA HABARI LEO


Na: Samuel Samuel,

Leo majira ya saa 6:30 mchana katika makao makuu ya klabu ya Yanga jijini Dar es salaam , katibu mkuu wa klabu hiyo ndugu Charles Boniface Mkwasa aliitisha mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu klabu hiyo .

Mkwasa alianza na pongezi kwa klabu yake kwa kuweza kutinga hatua ya nusu fainali kombe la ASFC baada ya kuibanjua Tanzania Prisons goli 3-0 mchezo uliopigwa jumamosi katika dimba la Taifa.

Mkwasa ametumia mkutano huo kueleza hatua ambayo klabu imechukua katika kuongeza mapato ya klabu hiyo kutokana na kulegalega kwa hali ya uchumi klabuni hapo .

Hatua iliyochukuliwa ni kufungua akaunti maalumu ambayo itawapa fursa wapenzi , wanachama, mashabiki na wadau wa timu hiyo kuichangia fedha klabu yao ili kuipa nguvu ya misuli ya kiuchumi.

" ni ombi la wanachama wenyewe kujitolewa kuichangia timu yao na sisi kama uongozi tumeona ni jambo lenye tija . Hii haina tafsiri ya kwamba klabu haina fedha na imekwama kabisa kujiendesha bali tumelipitisha ili kukidhi matakwa ya wengi . Si wote wanaokuja uwanjani au kulipia kadi kama sehemu ya kuongeza mapato ya klabu lakini kwa mfumo huu ambao tunaenda kuuzindua utatoa fursa kwa kila mdau popote alipo kuichangia klabu kama sehemu ya kujivunia timu hii na kusimama kama nguzo muhimu ya maendeleo ya klabu. Akaunti itafunguliwa kupitia Selcom " alieleza katibu huyo .

Sanjari na hilo , Mkwasa pia amegusia maandalizi ya timu kuelekea mchezo wa nusu fainali ASFC tarehe 30 April dhidi ya Mbao FC jijini Mwanza .

" tunaheshimu uwezo wa Mbao na sisi tunajipanga vyema kupata ushindi katika uwanja wa Kirumba . Benchi la ufundi baada ya droo ya jana na kujua mpinzani wetu ni nani , tayari wameanza mazoezi kujiandaa na mchezo huo . "

Droo ya nusu fainali ASFC ilifanyika jana jioni . Mabingwa hawa watetezi Yanga SC watawavaa Mbao FC na Simba SC watakwaana na Azam FC uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam tarehe 29 April 2017.

MUHIMU
Unaombwa kuichangia klabu hii kwa mtandao wowote wa simu unaotumia kwa kutumia kumbukumbu namba hii hapa chini :

Kumbu Kumbu namba ni  150334

Jina litasoma  YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB.

Imeandaliwa na Samuel Samuel

LIKE AND SHARE THIS POST ILI WATU WENGI WAPATE KUIONA AKAUNTI YA SELCOM NA KUICHANGIA KLABU

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search