BAGAMOYO NA MKURANGA 'KIDEDEA' MAAMBUKIZI MAPYA YA UKIMWI MKOANI PWANI

Wadau na wataalamu mbalimbali wa afya mkoani Pwani wakifuatilia jambo kwenye mkutano uliokuwa ukizungumzia utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Wadau na wataalamu mbalimbali wa afya mkoani Pwani wakifuatilia jambo kwenye mkutano uliokuwa ukizungumzia utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Mratibu wa TACAIDS Pwani na kaimu Dar es salaam Charles Kamugisha akizungumza jambo kwa waandishi wa habari.

Meneja wa takwimu mkoani Pwani,Kalisto Lugome akizungumza jambo kwenye mkutano uliokuwa ukizungumzia masuala ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
HALI ya maambukizi ya ukimwi mkoani Pwani ,imefikia asilimia 7.2 huku wilaya ya Bagamoyo na Mkuranga ikiwa inaongoza kimkoa.
Wilaya hizo zimetajwa kuongozwa kutokana na barabara kuu, uvuvi, utalii,biashara za ngono,vigodoro na baadhi ya mila na desturi.
Aidha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa watafiti wa ugonjwa wa Ukimwi mkoani humo wanaotarajia kuanza zoezi hilo hivi karibuni ili kupata takwimu sahihi .
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ,wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi .
Alieleza tafiti na takwimu sahihi zitasaidia kupanga mipango mizuri ya namna ya kuukabili ugonjwa na kujua ukubwa wa tatizo.
Ndikilo alisema utafiti wa namna hiyo nchini ni wa wanne hapa nchini ambapo utafiti wa wa kwanza ulikuwa 2003/2004, wa pili ulikuwa mwaka 2007/2008 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011/2012 ambazo zilikuwa zikihusisha watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49.
“Utafiti wa mwaka huu ni wa kipekee kwani utahusisha kaya zilizochaguliwa, rika zote kuanzia watoto hadi wazee,” alisema Ndikilo.
Alisema utafiti huo ni wa kwanza kukusanya taarifa zinazohusiana na maambukizi mapya ya vvu, kiwango cha vvu mwilini kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo, wastani wa maambukizi ya vvu kwa watu wa rika zote na wingi wa chembechembe za kinga mwilini.
Alieleza kiwango cha maambukizi ya VVU katika tafiti zilizopita kinaonekana kupungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003 hadi asilimia 5.1 mwaka 2011 na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango cha chini kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara .
Mhandisi Ndikilo alisema nchi za ukanda huo zina kiwango cha zaidi ya asilimia 10 wakina mama wakiwa na asilimia 59 kuliko akina baba.
Nae mratibu wa TACAIDS Pwani, Charles Kamugisha alisema maambukizi makubwa yapo kwenye barabara kuu kama vile Chalinze, Mdaula na Misugusugu.
Alisema makundi yanayoathirika kwa kiasi kikubwa ni pamoja na wanawake wanaofanya biashara ya ngono kwenye barabara hizo na vijana .
Meneja wa Takwimu mkoa wa Pwani Kalisto Lugome alisema ,zoezi hilo lilianza na kwa kuorodhesha kaya ambazo zitafanyiwa utafiti huo.
Alieleza,katika tafiti hizo wataanza kuhamasisha na kutoa elimu watu na kaya zilizochaguliwa kwenye zoezi hilo.
Lugome alisema baada ya hapo, ndipo zoezi la kufanya tafiti kupata takwimu muhimu ndio litaanza.
No comments:
Post a Comment