CCM Z’BAR YAWEKA WAZI MSIMAMO WAKE DHIDI YA CUF
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi CCM Zanzibar, kimeendelea kuweka wazi msimamo wake kuwa hakiwezi kukaa meza moja na CUF kuzungumzia Uchaguzi wa mwaka 2015 na Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK) bali kipo tayari kukaa na chama hicho kujadili changamoto zinazowakabili wananchi.
Msimamo huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Abdallah Juma Saadalla “Mabodi” katika Mahojiano Maalum kuhusu masuala ya hali ya Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii nchini huko Afisini Kuu CCM Kisiwandui, Unguja.
Alisisitiza kwamba mjadala wa mambo hayo, umefungwa toka Machi 20, mwaka 2015 katika Uchaguzi wa marudio, hivyo kwa sasa CCM inasimamia serikali zake zitekeleze kwa uhakika na haraka Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 12015/2020, kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Dkt. Mabodi alisema kitendo cha kuendelea kujadili Uchaguzi uliopita ambao mwanzo ulifutwa kisheria na kurudiwa tena ni kudhalilisha Katiba ya nchi, jambo ambalo CCM haipo tayari kwani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein na Watendaji wake wameingia madarakani kwa misingi ya Kidemokrasia Kanuni na sheria za nchi na Dunia yote inajua hivyo.
Hoja hizo zimekuja baada ya siku za hivi karibuni pindi ujumbe wa Ubalozi wa Marekani kufanya mazungumzo na Chama hicho, na baadae baadhi ya Magazeti na Mitandao ya kijamii kupotosha mazungumzo hayo kwa kudai kuwa upo uwezekano vya vyama hivyo viwili kurudi katika meza ya mazungumzo kujadili Suala la Uchaguzi uliopita na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia alisema Chama hicho kipo tayari wakati wowote kuzungumza na Chama chochote cha kisiasa, na nchi mbali mbali Duniani juu ya kujadiliana mikakati na mbinu endelevu ya kutatua matatizo na kero za wananchi hasa wa baadhi ya Majimbo ya Pemba yasiyokuwa na maendeleo licha ya kuwa na Wabunge wanaotoka CUF, waliowasusia wapiga kura wao na mzigo wote kuwaachia Wawakilishi na madiwani wa CCM pekee.
“ Naomba Wapinzani wetu waelewe kwamba Zanzibar ina mihimili mitatu ya Dola ambayo ni Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama, vyombo hivi vipo kisheria vikiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein na Baraza lake la Mawaziri, sasa mnataka tujadili nini tena.
Pia kwa lugha rahisi na inayoeleweka zaidi ni kwamba Safu hiyo itaendelea kubaki madarakani mpaka 2020, hakuna miujiza wala taifa lolote Duniani la kuingilia siasa zetu za ndani”., alisema Dkt. Mabodi na kuwataka wanasiasa kuwa wakweli na wenye utu na huruma za kupigania wapiga kura wao wawe na maisha mazuri, na kuondokana na siasa za jino kwa jino, chuki na migogoro.
Huduma za kijamii
Alisema serikali inayotokana na CCM kupitia Dkt. Shein imeimarisha huduma za afya sambamba na kuongeza vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na Pemba Hospitali ya Abdalla Mzee huku ikiboresha kitengo cha upasuaji wa matatizo ya Uti wa Mgongo, Kichwa kikubwa, Mishipa ya fahamu na saratani ya Ubongo matibabu hayo yote yanafanyika Zanzibar Mnazi Mmoja bure.
Kwa upande wa sekta ya elimu serikali imeimarisha ngazi za elimu ya Awali hadi Vyuo vikuu ambapo kwa sasa inazalisha wataalamu wa fani mbali mbali hapa nchi huku wengine wakipata mafunzo yao nje ya nchi.
Aidha kumeimarishwa Sekta za Uvuvi, Ufugaji na kilimo cha kisasa ambapo wananchi wanapata huduma za Pembe jeo na kwa gharama nafuu na bure kwa wakati mwingine , huku wakilimiwa na Matrekta ya kisasa.
Kwa upande wa miundo mbinu ya serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa viwanja vya ndege na bandari za kisasa na kuruhusu wawekezaji katika usafiri wa baharini na makampuni ya ndege huku imejenga barabara za kiwango cha lami Unguja na Pemba mjini na vijijini ili wananchi wapate unafuu wa kutoa mazao yao mashambani hadi sokoni kwa urahisi.
“ Wabunge wote ndani ya Bunge la jamhuri ya Tanzania wanapokea Mafao, sitahiki, mishahara na fedha za majimbo sawa , lakini cha kusikitisha wenzetu wanaporudi majimboni wanadai kuwa serikali ya CCM ndio yenye dhamana ya kutatua kero za wananchi, sio kwamba tumechoka tunaendelea kufanya na tunafanya mpaka katika makaazi yao.” Alisema Dkt. Mabodi na kuongeza kuwa wapinzani wanakimbia majukumu yao kwa kutotekeleza yale waliyowaahidi wapiga kura wao.
Hali ya Kisiasa Zanzibar.
Dkt. Mabodi alisema hali ya kisiasa Zanzibar kwa ujumla ipo shwari licha ya kuwepo kwa changamoto za baadhi ya wanasiasa kutokubali mambo mema yanayosimamiwa na CCM katika utekelezaji wake.
Lakini alieleza kwamba Chama hicho hakitochoka kuwaelimisha kwani baadhi yao tayari wameanza kuhama ndani ya CUF na kujiunga na CCM, katika maeneo mbali mbali nchini na hivi karibuni wamepokea wanachama Wapya zaidi ya 90 huko Jimbo la Makunduchi waliovutiwa na Sera, na siasa za Chama Cha Mapinduzi, waliodai kuwa wamechoshwa na sera za CUF zisizotekelezeka.
Alisema kwamba kila nchi duniani ina mifumo yake ya kiutawala hivyo katika ulimwengu wa Kidemokrasia lazima uwanja wa siasa uwe na faida na kasoro za hapo na pale kwani sehemu yoyote yenye pande mbili zinazopingana kimisimamo lazima hayo yatokee lakini ni mambo yanayozungumzika.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema SUK iliwekwa na wananchi wa Visiwa vya Zanzibar na wakati ukifika wakaamua wenyewe kuiondosha au ibaki na kueleza kuwa yeye sio mingoni mwa fikra za wapinzani wanaoamini kuwa Utulivu na Amani ya Zanzibar vipo kwa ajili ya mfumo huo bali anachokiamini ni kwamba Wananchi wamekuwa waelewa zaidi na kupima katika uzani kuwa ni siasa zipi wazifuate ndipo walipamua dhana hizo kwa kuzika siasa za Chuki na Marumbano.
“ Kipindi tupo katika SUK Zanzibar yalitokea matukio mengi ya kutisha Zanzibar ambayo kihistoria hayakuwahi kutokea na huwa sipendi kuyakumbusha ila nitatoa mifano, kuwa matukio hayo ni pamoja na kujitokeza vikundi vya Kihalifu kama Mbwa Mwitu, viongozi wa dini kuuawa na kumwagiwa Tindi kali pamoja, kuchomwa kwa Makanisa, kuchomwa kwa Matawi na Ofisi za CCM, uhalibifu wa miundombinu na baadhi ya wananchi kuigomea serikali.” Alifafanua Dkt. Mabodi na kuhoji kuwa vitendo hivyo wakati vinatokea Wenzetu tulikuwa katika serikali Kitaifa SUK, hakuna hata kiongozi hata mmoja aliyekemea wala kulaani uhalifu huo.
Siri ya CCM kuwa imara kwa miaka 4O.
Mwanasiasa huyo alisema kufanikiwa kwa Chama hicho kunatokana na radhi za Wazee wa Chama hasa wale walioasisi vyama vya ASP na TANU, ambao miongozo waliyoiacha mpaka sasa bado inaimarishwa tena kwa mifumo ya kisasa.
Pia alisema kwamba sababu nyingine ya kuaminika kwa chama hicho inatokana na muundo wake ambao umejitawanya kuanzia ngazi za mashina ( Nyumba kumi) hadi Taifa zote hizo zinakuwa na viongozi wanaochaguliwa Kidemokrasia hali ambayo ni tofauti na vyama vingine vilivyojenga safu za uongozi kwa ngazi za juu pekee.
Hali ya kiuchumi
Naibu huyo ambaye amewahi kufanya kazi katika taasisi za kimataifa, alisema kwamba uchumi wa Zanzibar unakuwa kwa kasi kutokana na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato, unaotokana na usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi zinazoendana na matakwa ya sasa ya kuelekea katika falsafa za Zanzibar yenye viwanda.
Aliwashauri wananchi kutumia vizuri fursa na mazingira bora ya kimiundo mbinu yaliyowekwa na serikali kwa kufanya kazi kwa bidii hasa zile za uzalishaji mali ili waweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aliwaomba Wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Marais wa pande zote mbili ambao ni Rais wa Zanzibar , Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kasi zao nzuri za kiutendaji juu ya maendeleo ya nchi.
Aidha alisema Zanzibar imepata neema ya Uchimbaji na utafutaji wa rasilimali za Mafuta na gesi asilia ambazo kwa sasa tayari zimeanza kwa nchi nzima, hivyo wananchi watoe ushirikiano kwani fursa hiyo ni moja ya vitega uchumi muhimu vya kitaifa, lakini wasisahau kujiimarisha katika sekta za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji.
Mgogoro unaoendelea ndani ya CUF kwa sasa
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema hawezi kuzungumzia sana mgogoro huo kwani haubebi dhamira ya kutatua kero za Wanzania, bali unaendelea kukuwa kutokana na baadhi ya viongozi wa Chama hicho kugubikwa na uchu wa madaraka na Utawala huku wakisahau kwamba fursa hizo zinatokana na majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.
Aidha alisema huu ndio wakati mwafaka wa Watanzania kupima siasa za Vyama vya Upinzani na badala yake wakafanya maamuzi sahihi ya kuviacha na kujiunga na CCM chama ambacho kauli na vitendo vyake vinahimiza Amani, Mshikamano na Umoja sambamba na kueneza sera za maendeleo kwa wananchi wote.
No comments:
Post a Comment