HUU UBABAISHAJI SASA!!
HUU UBABAISHAJI…………………
1. Uongozi wa mpira, Kama wapiga ramli,
Wananitia hasira, Kwakweli sio wakweli,
Timu ikiwa fukara, Wanai chinjia mbali,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
2. Kwa manufaa ya nani, Hawa ndumila kuwili,
Mara pointi mezani, Na mara wamebadili,
Mnatumia kanuni, Au ni zenu akili,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
3. Kanuni zasema wazi, Au mmezibadili,
Kadi tatu hauchezi, Mechi moja sio mbili,
Sasa yenu maamuzi, Ya sasa si ya awali,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
4. Tunaweka ushabiki, kama hatuna akili,
Tunaendeleza chuki, Na kupakana asali,
Wabebe hawabebeki, Nje hawafiki mbali,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
5. Mpira bongo fitina, Hata ushindi halali,
Ubingwa wa kupeana, Zaonekana dalili,
Kutwa ni kufungiana, Unaposema ukweli,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
6. Viongozi wote yanga, Simba hana afadhali,
Hata washika kipyenga, Nawao ni kandambili,
Soka letu ni majanga, Heri tucheze kamali,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
7. Wote ni kabila moja, Wallah hatukubali,
Tena ujanja ujanja, Hiyo ni yao asili,
Kanuni wanazivunja, Wala wao hawajali,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
8. Mungu akipanga lake, Hayupo wa kubadili,
Simba huu mwaka wake, Mabingwa si namba mbili,
Apewe pointi zake, Nayo matatu magoli,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
9. Mpeni yanga ubingwa, Muone yanayojili,
Bao nne atadungwa, ende kufilia mbali,
Mechi za nje hufungwa, Huona vimulimuli,
Huu ubabaishaji, Kwa manufaa ya nani.
10. Mimi hapa naishia, Mimi ni msema kweli,
Hata mkinifungia, Wallah mimi sijali,
Maoni nimeyatoa, Na kuonyesha dalili,
Kunya basi anye kuku, Kinya bata kaharisha.



No comments:
Post a Comment