#LHRC WATOA TAMKO UVAMIZI MKUTANO WA CUF

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunasikitishwa na mlolongo wa matukio ya uvunjifu wa amani yanayoshamiri siku hadi siku. Kituo tunashitushwa na matukio hayo yanayodunisha amani na kumomonyoa misingi ya demokrasia nchini Tanzania.

Tukio la uvamizi katika mkutano wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) uliopelekea kupigwa na kujeruhiwa kwa wanachama na waandishi wa habari huko Mabibo, Ubungo, Dar es Salaam limezidi kuzua mjadala katika jamii juu ya hatma ya hali ya usalama kwa taifa. Tunatoa pole kwa waandishi wa habari, viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF).
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona kuwa huu ni ukiukwaji mkubwa wa misingi ya demokrasia kwa kuzingatia aina ya shughuli iliyokuwa ikiendelea. Pia tukio hilo limezua hofu juu ya usalama wa wanahabari wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo linazorotesha haki ya kupata taarifa.

Tunaitaka serikali kutofumbia macho matukio haya yanayoota mizizi kwani kwa kufanya hivyo ni kuhalalisha vitendo vya kihuni na kuruhusu uvunjwaji wa sheria kiholela.
Kwa kuzingatia umuhimu wa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kukusanyika kituo cha sheria na haki za Binadamu tunapendekeza yafuatayo;

1.       Msajili wa vyama vya siasa kuhakikisha ustawi mzuri wa vyama vya siasa kwa kutatua migogoro iliyopo ndani na baina ya vyama vya siasa ili kuepusha matukio ya uvunjifu wa amani na kudumisha ustawi wa demokrasia.
2.       Serikali kuhakikisha usalama kwa raia wanapokuwa kwenye shughuli zao ili kuepusha hofu kwa wananchi.
3.       Vyama vya siasa kutumia uhuru wao kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa bila kusababisha uvunjifu wa amani.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunataamali jamii yenye kuheshimu na kulinda haki za binadamu.

Imetolewa na:
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search