SAMIA AHIMIZA WANAFUNZI KUPENDA MASOMO YA SAYANSI!
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahimiza wanafunzi kote nchini kupenda kusoma masomo ya sayansi hasa watoto wa kike ili taifa liweze kujitosheleza kwa wataalamu wa fani mbalimbali nchini hasa wakati huu ambao Taifa linaelekea kwenye uchumi wa Viwanda.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mahafali ya Pili ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wa shule ya sekondari ya WAMA- NAKANYAMA Jijini Dar es Salaam, mahafali ambayo imehudhuriwa na wake wa Marais wastaafu.
Makamu wa Rais amesema haitapendeza hata kidogo ajira nyingi nchini kuchukuliwa na wataalamu mbalimbali wa mataifa ya nje hasa kipindi hiki wakati Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda hivyo amesisitiza wanafunzi wajikite kwenye kusoma masomo ya sayansi ili taifa liweze kujitosheleza kwa ajili ya manufaa ya maendeleo ya taifa.
Amesema katika kuhakikisha taifa lipata wanasayansi wengi, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa maabara na kununua vifaa vya maabara ili kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kupenda kusoma masomo ya sayansi kote nchini.
Makamu wa Rais pia amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Tano inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano -TEHAMA- katika shule za Sekondari na kujenga maabara za kompyuta nia ikiwa ni kuongeza wataalamu wa fani hiyo nchini.
Kuhusu mila na desturi kandamizi kwa wanawake na wasichana zilizopo kwenye baadhi ya jamii nchini, Makamu wa Rais ameitaka jamii kukomesha mila hizo na iwashirikishe wanawake katika mipango na mikakati ya maendeleo ya nchi kwani watakuwa ni chachu ya maendeleo katika jamii husika.
"Wote tunajua wanawake ni chachu na kiungo muhimu katika maendeleo ya jamii, Taifa na Dunia kwa ujumla hivyo ni wajibu wa jamii kushirikisha wanawake katika kupanga na kutekeleza shughuli za maendeleo kote nchini" amesisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais pia ameipongeza Taasisi ya Wanawake na Maendeleo - WAMA- kwa kujenga shule Mbili za Sekondari na kusomesha watoto wanaotoka kwenye familia maskini na yatima na kusema huo ni mfano wa kuingwa na wadau wengine wa maendeleo katika kusaidia kundi hilo ili watoto wanaotoka kwenye familia maskini nao waweze kuapata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Kuhusu changamoto zinazoikabili shule ya WAMA - NAKAYAMA, Makamu wa Rais ameahidi kushughulikia changamoto hizo ikiwemo uhaba wa maji, ubovu wa barabara kuelekea kwenye shule hiyo na tatizo la uhaba wa mabweni
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WAMA na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mama SALMA KIKWETE amesema aliamua kuanzisha taasisi hiyo ambayo inamiliki shule Mbili mpaka sasa ili kusaidia watoto wa maskini na yatima kupata elimu bure ambapo mpaka sasa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaliohitimu katika shule hizo ambao wamejiunga na masomo ya elimu ya juu.
Mama Salma Kikwete ameshukuru ushirikiano mkubwa anaopata kutoka Serikalini unaolenga kuhakikisha shule zinazoendeshwa na taaisisi hiyo ikiwemo ya Wama - Nakayama zinafanya vizuri
Bbc swahili
No comments:
Post a Comment