#SPORTS #MAKALA: HEKAYA ZA ABUNUASI KATIKA SOKA LA TANZANIA NA UTUNZI WA SHAIRI YANGA INABEBWA...


Kabla ya kuendelea kwa soka barani ulaya mwishoni mwa miaka ya 70 na kuanza kuuteka ulimwengu kwa ligi zao bora na vilabu mbalimbali vilivyoanza kujizolea mashabiki kila pembe ya dunia mfano , Liverpool , Barcelona , Juventus , Manchester, Real Madrid na nyinginezo  dunia iligawanyika pande mbili kisoka ngazi ya kimataifa.

Wapo waliokuwa mashabiki wa Brazil wakitembea vyema na mafanikio ya kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo al maarufu kama selecao na wapo waliokuwa wakishabikia  soka la Argentina .

Brazil ilijengwa vyema na wakali wake kama Pele , Garincha , Zicco na wengine huku Argentina ikijizolea mashabiki kwa umaridadi wa kikosi hicho chini ya mkongwe Maradona . Ushindani huu ukaitengenezea dunia wapinzani wa jadi na kila bara kujikuta lina wapenzi wa timu hizi mbili lakini Brazil ikiwa na wapenzi wengi zaidi .

Hali hii katika soka haikwepeki na ipo siku zote na itaendelea kuwepo . Licha ya Liverpool kutofanya vyema pale England kwa maana ya kutochukua kikombe cha ligi kuu toka 1985 lakini bado wakongwe hao wana mashabiki wengi tu kama ilivyo kwa Manchester United.

Hapa nchini tumegawanyika pande kuu mbili yaani Simba SC na Yanga SC . Baadhi ya takwimu zinaonesha Yanga ina mashabiki takribani asilimia 40%, , Simba 25% , asilimia 10% timu nyingine nje ya Yanga na Simba na zilizobaki si wadau  wa soka kwa dhana ya ushabiki.

Kwa takwimu kama hizi ambazo si rasmi lakini hazipo mbali na ukweli unashangaa nini kuona viongoI wengi wa nchi au chama cha soka wanatoka Yanga ?

Labda niseme jambo moja , ukiondoa viongozi wa kisiasa ndani ya serikali kuna viongozi na wafanyakazi lukuki ambao si wapenzi au wanachama wa CCM licha ya kuitumikia serikali inayoongozwa na chama hicho . Kuna wakati unafika  mapenzi binafsi kando na kinachofanya kazi ni taaluma yako.

Sasa kwa mifano kama hii tuache kuwahukumu viongozi wetu kwa kupitia unasaba wao kwa timu wanazozipenda au waliwahi kuzitumikia . ViongoI hawa wana dhamana ya kuliongoza shirikisho letu la soka na si kuiongoza Yanga .

Tuache tabia ya kuwaorodhesha viongozi na timu wanazoshabikia na kujenga hoja wapo kwa ajili ya kuzipendelea timu zao pendwa . Hii inachangia kukuza imani hasi ndani ya jamii kuhusu utendaji wao na maamuzi yao .

Ni ukweli wapo viongozi wasiojielewa wanaoshindwa kutenganisha kazi na mahaba yao kwa timu zao lakini si vyema kutoa mjumuisho .

Malinzi na wenzake tuwahukumu kwa mengine lakini kwa hili la Yanga hebu muacheni.

Sasa unawezakuta raisi wa FIFA ni miongoni mwa wapenzi wa Brazil au Argentina je azibebe katika maamuzi?!

Shairi la " Yanga inabebwa" liachwe maana muda si muda litageuka sumu katika soka la nchi hii.  Azam akitafuta kujiimarisha katika soka la nchi hii naye alikuwa muhanga wa kauli hizi na bado mpaka leo muhanga wa kauli hizi , je utafiti unafanyika kwa kina???!

Mwisho wa siku tuzione hizi ni hekaya za abunuasi katika soka letu . Kikubwa kila idara ifanye kazi kwa uadilifu mkubwa na tuache zana ya kuchafua timu kwa dhana ya kubebwa kila mara na viongozi husika .

Samuel Samuel

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search