Watanzania kufanya miamala ya kifedha kupitia Halopesa na NMB
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu ya Halotel Le Van Dai akibadilishana hati za makubaliano na Kaimu Mkuu wa Akiba za Watu Binafsi wa Benki ya NMB, Boma Raballa ambapo wateja wa Halotel watafaidika na huduma za kifedha za Halopesa kwa ataweza kuchukua na kuweka fedha zake kutoka katika akaunti yake ya NMB. Makubaliano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Ofisa Mwendeshaji wa Halopesa, Henry Mavula na kulia ni Meneja wa Huduma za Ziada wa benki ya NMB,Stephen Adili.
KATIKA kufanikisha azma ya kupanua wigo wa huduma za kifedha kwa wananchi wenye vipato tofauti, kampuni ya mawasiliano ya Halotel na benki ya NMB zimeingia katika ushirikiano utakao wawezesha mamilioni ya watanzania kunufaika na huduma za kifedha nchi nzima.
KATIKA kufanikisha azma ya kupanua wigo wa huduma za kifedha kwa wananchi wenye vipato tofauti, kampuni ya mawasiliano ya Halotel na benki ya NMB zimeingia katika ushirikiano utakao wawezesha mamilioni ya watanzania kunufaika na huduma za kifedha nchi nzima.
Hatua hii itawawezesha watanzania wengi zaidi kufikiwa na huduma za kifedha kwa njia ya mtandao ikiwa ni sehemu ya kufanikisha azma ya serikali ambayo inazitaka taasisi mbalimbali za kifedha kuwafikia wananchi na huduma zao hasa kwa maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel, Le Van Dai amesema kuwa ni hatua nyingine kubwa katika utoaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi ambapo sasa huduma ya Halopesa itakuwa imeunganishwa na benki ya NMB ili kuwawezesha wateja kufanya miamala kwa urahisi zaidi.
Dai ameendelea kuwa ushirikiano huo, umeunganisha taasisi kubwa zenye wateja wengi na zilizosambaa kwa kiasi kikubwa nchini. Tunatarajia huduma hii itapunguza kadhia kwa watumishi wa taasisi za umma, wakiwemo walimu na watu wa sekta zingine wakiwemo wakulima, wavuvi na wafanya biashara wanaoishi vijijini ambako huduma za kibenki hazijafika kote. Maeneo haya kwa kiasi kikubwa hutegemea njia ya simu za mkononi kuweza kutoa fedha au kuweka kwa njia ya haraka na usalama zaidi.
“Ushirikiano huu ni wa kipekee katika kurahisisha maisha ya watanzania ambao wamekuwa wakipata tabu kupata huduma za kifedha kutokana na maeneo wanayoishi. Sisi kama Halotel hadi sasa tumewafikia watanzania kwa zaidi ya asilimia 95. Hivyo ni dhahiri kwamba wateja watakaojiunga nasi wataweza kutoa au kuweka fedha huko huko waliko kupitia kwa mawakala wetu ambao wameenea nchi nzima,” aliongezea Dai.
“Tunatambua changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiwasibu Watanzania hasa wa kipato cha chini. Kwani wengi wao walikuwa wanakwama kuweza kupata huduma za kifedha kutokana na miundombinu kutowafikia. Mpaka hivi sasa Halotel ina mawakala zaidi ya 30,000 walioenea nchi nzima. Hii itawawezesha wakazi wa maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na mawasiliano kabisa au huduma za kibenki sasa kuweza kupata huduma za kifedha kupitia simu zao za mkononi,” alimalizia Naibu Mkurugenzi wa kampuni hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Huduma Binafsi za Kibenki wa NMB, Boma Raballa, amesema ushirikiano huo ni mafanikio mengine makubwa ya kibiashara kwao hususani katika kupanua wigo wa huduma zake na namna itakavyoweza kuunganisha teknolojia ili kuwarahisishia watanzania kupata huduma za kifedha popote walipo.
“Benki ya NMB ni ya kwanza kutoa huduma za kipekee na zenye ubunifu wa hali ya juu na tunaamini ushirikiano huu utatuwezesha kuwafikia watanzania wengi zaidi. Watanzania wanahitaji huduma za kifedha muda wowote na mahali popote walipo. Hivyo kuja kwa ushirikiano huu kutawaletea uhakika wa kupata fedha tena kwa njia rahisi kabisa kwa kutumia simu zao za mkononi maana sio muda wote watakuwa karibu na mashine zetu za kutolea fedha (ATM) au matawi ya benki yetu,” alisema Raballa
“Kwa kushirikiana na Halotel tunaamini tutakuwa tumefanikisha lengo la serikali na benki yetu kwa ujumla katika kuwafikia watanzania wengi zaidi. Hii inamaanisha kuwa wateja wa kampuni hizi mbili ambazo hawajafikia na huduma aidha za NMB au Halotel basi watafikiwa kwa pamoja. Mbali na kurahisisha huduma lakini pia itasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kuboresha na kurahisisha hali ya maisha na uchumi kwa watanzania, yaani kwa watoa na wapokea huduma,” aliongezea Raballa.
No comments:
Post a Comment