Mtambo wa Marekani kuzuia makombora ya Korea Kaskazini waanza kazi

Mtambo wa Thaad umewekwa kuzuia makombora kutoka Korea Kaskazini
Jeshi la Marekani limesema mfumo wake wa Thaad wa kutoa kinga dhidi ya makombora umeanza kufanya kazi nchini Korea Kusini.
Msemaji wa jeshi hilo amesema mtambo huo sasa una uwezo wa kuzuia makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini na pia kuilinda Korea Kusini.
Lakini maafisa wameambia wanahabari kwamba itachukua miezi kadha kabla ya mfumo huo katika kutumika kikamilifu.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikitanga katika rasi ya Korea, huku Korea Kaskazini ikiendelea kutoa vitisho mara kwa mara.
Marekani nayo imetuma kundi la meli za kivita pamoja na nyambizi katika rasi hiyo.
Jumatatu, ndege mbili za kuangusha mabomu za Marekani zilifanya mazoezi ya pamoja na jeshi la wanahewa la Korea Kusini, operesheni ambayo Marekani ilisema ilikuwa ya kawaida.
Mtambo wa Thaad, ambao kwa kirefu husimamia Terminal High Altitude Area Defence, ulianza kuwekwa wiki iliyopita katika eneo ambalo zamani lilikuwa uwanja wa gofu katika eneo la Seongju katikati mwa Korea Kusini.
Baadhi ya raia wa Korea Kusini waliandamana kuupinga.
Wengi wa wenyeji wanaamini mtambo huo unaweza kulengwa na adui na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wanaoishi hapo karibu.
China pia imepinga kuwepo kwa mtambo huo - ikisema uwezo wake wa rada huenda ukahitilafiana na operesheni zake za kijeshi.
Msemaji wa jeshi la Marekani aliyepo Korea Kusini alisema mtambo huo wa Thaad sasa "unafanya akzi na una uwezo wa kuzuia makombora yanayorushwa kutoka Korea Kaskazini na kuilinda Jamhuri ya Korea."
Baadhi ya wakazi Korea Kusini waliandamana kupinga kuwekwa kwa mtambo huo
- bbc swahili

About Author Matukio360

Matukio360 ni sehemu pekee inayokuletea matukio ya moto moto kutoka pande zote za dunia katika wakati ule ule yalipotokea yaani mubashara. Habari ni za uhakika na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina na kuandikwa kwa ueledi mkubwa na sio ukanjanja. Usibanduke katika ukurasa huu wa Matukio360, wajulishe na marafiki zako sasa wajipatie habari za uhakika.

No comments:

Post a Comment

Leo leo Plus

Start typing and press Enter to search