Upambe: ADC washangazwa na 'upambe' wa CHADEMA kwa Chama cha Wananchi CUF.. wakemea mauaji ya Kibiti... #share

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu
Taifa wa chama hicho, Doyo Doyo aliyesema hali ya kisiasa nchini si nzuri na
kwamba Serikali kwa kuendelea kuzuia shughuli za kisiasa ni tishio kwa vyama
kama ADC akisema huenda vikafa.
“Hali ya kisiasa sio nzuri sana, kuna hali ya kutopata uhuru
wa kufanya siasa hasa katika upande wa vyama vya upinzani katika nchi yetu. Kuzuiwa
kufanya mikutano ya kisiasa, makongamano na kadhalika, hii inaua vyama vya
siasa,”alisema na kuongeza:
“ADC inamuomba Rais John Magufuli atuachie tufanye mikutano
kwani jambo hili ni takwa la kisheria.”
Akizungumzia usalama nchini alisema hawaridhishwi na taarifa
za mauaji yanayoendelea Kibiti mkoani Pwani akisema yanatia doa Taifa, ambapo
aliiomba Serikali kujipanga upya na kuweka mkakati madhubuti ya kukabiliana na
wahalifu.
Kuhusu migogoro ndani ya vyama vya siasa Doyo alisema ADC
kinashangazwa na mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) kushindwa kupatiwa
ufumbuzi wa haraka hali inayofanya wanachama wake kuanza kukata tamaa.
Alisema ADC unachukizwa na hali hiyo kwani kuendelea kwa
mgogoro huo kwa muda mrefu ni kunadhoofisha afya ya upinzani katika macho ya Watanzania.
“Nawaomba Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba
wakae pamoja ili kumaliza tofauti zao,” alisema Doyo.
Aidha, alieleza kushtushwa kwa ADC na matamko mbalimbali ya
viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuingilia mgogoro huo
wa CUF.
Doyo aliwashauri Chadema kuacha mara moja kuingilia mgogoro
usiowahusu akidai kitendo hicho cha kuingilia mgogoro huo usiowahusu ni mkakati
wa kisiasa wa kujitengenezea hati miliki ya kisiasa nchini, lakini pia kinaweza
kuhatarisha amani.
Hata hivyo, Doyo alisema alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi
zake anazofanya kuzuia rasilimali za nchi hasa kwa kitendo cha kuwasilisha
miswada kwa hati ya dharura bungeni ili kufanyiwa marekebisho ya sheria.
No comments:
Post a Comment